China yataka kuweko amani jumuishi na athirifu huko Palestina
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa China ametoa mwito wa kuwepo amani jumuishi na athirifu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Wang Yi amesema hayo katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari akiwa na mwenyeji wake Sameh Shoukry, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Misri na kueleza kwamba, China imefanya kila juhudi kulinda usalama wa raia na imefanya juhudi zisizo na kikomo kuhimiza suluhisho la kina, la haki na endelevu kwa suala la Palestina.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China ameongeza kusema kuwa, kipaumbele kikubwa kwa sasa ni kumaliza mzozo wa Ukanda wa Gaza katika muda mfupi iwezekanavyo, na kuzingatia kutumwa mara moja kwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda huo kama jukumu la kimaadili la nchi zote.
Kadhalika amesema, hivi karibuni China itatuma shehena ya tatu ya misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.
Akisisitiza kwamba matakwa ya wananchi wa Palestina kuhusu mustakbali wa Ukanda wa Gaza yanapaswa kuheshimiwa kikamilifu, Waziri wa Mambo ya Nje wa China amesema: Usitishaji mapigano na kusimamisha vita ni matakwa ya kimsingi ya Gaza na kaulimbiu ya "Wapalestina watawale Palestina" ndio msingi wa kujadili mustakabali wa Gaza.
Akiwa nchini Misri, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa China amekutana na kufanya mazungumzo pia na Ahmad Abul-Gheit, Katibu Mkuu Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika makao makuu ya umoja huo mjini Cairo ambapo wawili hao wamejadili na kubadilishaana mawazo kuhusiana na masuala mbalimbali yakiwemo mmatukio ya Gaza.