UNRWA: Wapalestina 100,000 wameuawa, kujeruhiwa au kutoweka huko Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i108062-unrwa_wapalestina_100_000_wameuawa_kujeruhiwa_au_kutoweka_huko_gaza
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) amesema kuwa karibu asilimia tano ya wakazi wa Ukanda wa Gaza ama wameuawa au kujeruhiwa au wametoweka.
(last modified 2024-02-06T04:45:30+00:00 )
Feb 06, 2024 04:45 UTC
  • UNRWA: Wapalestina 100,000 wameuawa, kujeruhiwa au kutoweka huko Gaza

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) amesema kuwa karibu asilimia tano ya wakazi wa Ukanda wa Gaza ama wameuawa au kujeruhiwa au wametoweka.

Philippe Lazzarini amesema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X kwamba: "Katika miezi 4 ya vita, karibu watu 100,000 wa Gaza wameuawa, kujeruhiwa au kutoweka."

Ameongeza kuwa, zaidi ya asilimia 80 ya watu milioni 2.3 wamekimbia makazi yao, wengi wao mara kadhaa.

Lazzarini  amesema: "Usitishaji mapigano umechelewa; njia tofauti inahitajika kwa ajili ya watu wa Gaza, Israeli, mahali pengine katika kanda hii na kwingineko." 

Matamshi haya ya Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) yanakuja siku chache baada ya shirika la kutetea haki za binadamu la Euro-Med Human Rights Monitor lenye makao yake makuu mjini Geneva kutoa ripoti ya kutisha kuhusu mlolongo wa vifo na uharibifu mkubwa uliosababishwa na miezi minne ya vita vya mauaji ya kimbari yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo imesema: "Wapalestina wapatao 110,000 wanaripotiwa kuuawa, kutoweka na kujeruhiwa, na kuwaacha wengi wakiwa na ulemavu wa muda mrefu miezi minne baada ya kuanza mauaji ya kimbari ya Israel katika Ukanda wa Gaza".

Gaza

Kwa mujibu wa ripoti ya Euro-Med, idadi hiyo inajumuisha jumla ya vifo 35,096 -- 32,220 kati yao wakiwa ni raia - ikiwa ni pamoja na watoto 12,345, wanawake 7,656, wafanyakazi wa afya 309, wafanyakazi wa ulinzi wa raia 41, na waandishi wa habari 121.

Euro-Med imesema idadi ya waliojeruhiwa katika kipindi chote cha vita vya Israel ni 67,240, wakiwemo mamia ambao wamepata majeraha mabaya.

Euro-Med imeongeza kuwa kuendelea kwa jinai za utawala huo ni "kinyume cha sheria za kimataifa za kibinadamu, [na] Mkataba wa Geneva wa 1949, na ni sawa na uhalifu wa kivita kwa mujibu wa Mkataba wa Roma, unaoongoza Mahakama ya Kimataifa ya Jinai."