OCHA: Yamkini Israel inatenda uhalifu wa kivita huko Rafah
Hatua yoyote ya utawala haramu wa Israel ya kuendeleza uvamizi wake kamili wa Gaza hadi katika mji wa kusini wa Rafah wenye msongamano mkubwa wa watu inaweza kusababisha uhalifu wa kivita ambao lazima uzuiwe kwa gharama yoyote.
Hayo ni kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura OCHA.
Akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva Uswisi msemaji wa OCHA Jens Laerke amesema “Sisi kama Umoja wa Mataifa na Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa tunaweza kushuhudia na tunaweza kuweka wazi kile ambacho sheria inasema, "chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, ulipuaji wa mabomu katika maeneo yenye watu wengi unaweza kuwa uhalifu wa kivita.”
Hatua hiyo inafuatia OCHA kuripoti “kuongezeka kwa mashambulizi” katika mkoa wa Rafah siku ya Jumapili na Jumatatu. Wakati huo huo, maelfu ya watu wa Gaza wanaendelea kumiminika mjini Rafah, wakiwemo wengi waliokimbia mapigano makali huko Khan Younis.
Matokeo ya msururu huo wa watu ni kwamba idadi ya watu wa Rafah imeongezeka mara tano tangu utawala haramu wa Israel uanzishe vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza mnao 7 Oktoba, 2023.
Laerke alisema: “Nataka ieleweke wazi, kuongezeka kwa uhasama huko Rafah katika hali hii kunaweza kusababisha idadi kubwa ya raia kupoteza maisha yao na lazima tufanye kila linalowezekanalo kuzuia hilo."
Wapalestina zaidi ya 27,000 wameuliwa shahidi na wengine zaidi ya elfu 67 wamejeruhiwa tangu utawala wa Kizayuni uanzishe vita dhidi ya Ukanda wa Gaza mwezi Oktoba mwaka jana huku asilimia 85 ya wakazi wa eneo hilo wapatao milioni 2.3 wakibaki bila makazi.