Khalid Mash'al: Karibuni hivi, vita vya miezi sita vitamvunja adui Mzayuni
(last modified Sun, 14 Apr 2024 02:31:03 GMT )
Apr 14, 2024 02:31 UTC

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya ughaibuni ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS Khaled Mash'al, amepongeza istiqama ya kishujaa ya Ukanda wa Ghaza na kusisitiza kuwa vita vya miezi sita wanavyopigana Wapalestina na utawala wa Kizayuni wa Israel "karibuni hivi vitamvunja adui Mzayuni".

Mash'al ameyasema hayo katika hafla iliyofanyika katika mji mkuu wa Qatar wa Doha kuwaomboleza jamaa wa familia ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniya, waliouawa shahidi katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya kambi ya wakimbizi ya al-Shati kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza siku ya Jumatano.
 
"Hii sio raundi ya mwisho," amesisitiza Mash'al, akimaanisha Muqawama unaoendelea wa Wapalestina dhidi ya uvamizi wa utawala wa Kizayuni, na akaongezea kwa kusema: "ni raundi muhimu katika njia ya kuikomboa Palestina na kuushinda mradi wa Kizayuni."
 
Wakati huohuo, Msemaji wa Hamas Abdul Latif al-Qanou amesema utawala haramu wa Israel umekiuka na kukanyaga kanuni zote za kibinadamu na sheria za kimataifa.

Al-Qanou ameeleza hayo katika mahojiano na televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon na kufafanua kwamba, utawala wa Kizayuni unaokalia ardhi kwa mabavu umeshadidisha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wakati wa Sikukuu ya Idul-Fitr.

Msemaji wa Hamas amesema: mamia ya watu wameuawa huku magari ya raia, masoko yaliyofurika watu na nyumba za makazi vikiripuliwa kwa mabomu na vikosi vya wavamizi bila kujali hata kidogo hisia za kidini za Waislamu wala kuheshimu mila zao".
 
Abdul Latif al-Qanou ameendelea kueleza kwamba: wavamizi hao wa Kizayuni watenda jinai wameudharau mwezi mtukufu wa Ramadhani na sikukuu ya Idul-Fitr, na badala yake wameshamirisha mauaji ya raia.
Amesema: "wamefanya jinai na uhalifu zaidi kwa kukiuka kanuni zote za kimataifa na za kibinadamu".../

 

Tags