Misri: Gaza imefikia katika ukingo wa njaa
Mwakilishi wa Misri katika Umoja wa Matiafa amesema kuwa hali ya mambo katika Ukanda wa Gaza imefikia katika ukingo wa njaa.
Osama Mahmoud Abdulkhaliq, Mwakilishi wa Kudumu wa Misri katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa Cairo kwa mara nyingine tena inapinga mashambulizi ya Israel huko Ukanda wa Gaza na kusisitiza juu ya ulazima wa kusimamishwa oparesheni za kijeshi za utawala wa Israel unaotekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza.
Abdulkhaliq ameendelea kubainisha kuwa: Kuendelea mashambulizi ya Israe dhidi ya Gaza kumesitisha huduma za uokoaji na misaada ya kibinadamu katika eneo hilo. Mwakilishi wa Kudumu wa Misri katika UN ameongeza kuwa: Yale yanayojiri sasa katika mji wa Rafah ni jinai dhidi ya binadamu na kwamba jamii ya kimataifa inabeba dhima ya suala hilo.
Abdulkhaliq amesisitiza kuwa, huduma za kibinadamu zitaendelea huko Gaza iwapo Israel itawajibika na kusitisha mashambulizi yake.
Baraza la Mawaziri la Vita la utawala wa Kizayuni tarehe Sita mwezi huu (Mei) liliidhinisha kutekelezwa mashambulizi dhidi ya mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza; ambapo jeshi la Israel lilianza kuushambulia mji huo Jumanne Mei Saba.