Walimwengu waandamana wakilaani mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza
Maandamano ya kupinga na kulaani mauaji ya kimbari ya utawala ghasibu wa Kizayuni katika ukanda wa Gaza yanaendelea kufanyika katika nchi tofauti za dunia.
Wafuasi wa Palestina katika nchi mbalimbali za dunia, ikiwa ni pamoja na Uholanzi, Tunisia, Marekani, Uingereza, Hispania, Ufaransa, Italia, Kanada, Ujerumani na Morocco, wameandamana na kutangaza himaya na uungaji mkono wao kwa Palestina na Ukanda wa Gaza.
Waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina katika nchi tofauti za dunia huku wakiwa wamebeba bendera ya Palestina na kulaani jinai za utawala dhalimu wa Kizayuni wa Ukanda wa Ghaza hususan kambi ya Nuseirat wametaka kukomeshwa vita vya utawala ghasibu wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.
Jinai iliyofanywa na Marekani na Wazayuni kwenye kambi ya wakimbizi Wapalestina ya Nuseirat katika Ukanda wa Ghaza inadhihirisha zaidi, kuliko jambo jengine lolote, kuendelea kukashifika na kuaibika kimaadili Washington na Tel Aviv.

Siku ya Jumamosi tarehe 8 Juni, jeshi la utawala wa Kizayuni liliendeleza jinai zake za kinyama dhidi ya raia wasio na hatia katika Ukanda wa Ghaza, kwa kufanya shambulio la kiwendawazimu dhidi ya kambi ya Nuseirat katikati mwa Ghaza kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani.
Duru za tiba za Palestina zimetangaza kuwa, idadi ya waliouawa shahidi katika jinai hiyo iliyofanywa na adui Mzayuni huko Nuseirat katikati mwa Ukanda wa Ghaza imefikia watu 274 na idadi ya waliojeruhiwa imefikia watu 698, ambapo baadhi yao wako mahututi na wengine wengi wangali wako chini ya kifusi.