Jun 16, 2024 10:00 UTC
  • Wapalestina waswali Swala ya Iddi Masjidul Aqsa licha ya mbinyo

Makumi ya maelfu ya Wapalestina wameshiriki katika Swala ya Iddul Adh'ha iliyosaliwa leo kwenye Msikiti wa al-Aqsa mjini Baitul Muqaddas, licha ya kuwekewa vizuizi na kukabiliwa na hatua kali za kiusalama zilizochukuliwa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika mji huo unaoukalia kwa mabavu.

Iran Press imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, zaidi ya waumini 40,000 wa Kipalestina wamesali Swala ya Iddi hii leo katika Msikiti wa al-Aqsa katika mazingira ya kuogofya ya ulinzi mkali na msharti magumu yaliyowekwa na utawala ghasibu wa Israel kwa ajili ya kuingia katika mji wa Baitul Muqaddas.

Licha ya wanajeshi makatili wa Israel kuweka vizuizi vingi na vikali, lakini maelfu ya Wapalestina wamehakikisha wanafika kwenye Msikiti wa al-Aqsa na kutekeleza ibada ya Swala ya Idul Hajj ambayo ni katika Sunna zilizotiliwa mkazo mno na dini tukufu ya Kiislamu.

Aidha Swala ya Iddi imeswaliwa katika Msikiti wa Nabii Ibrahim AS mjini al-Khalil, huku maelfu ya Wapalestina wengine wakitekeleza ibada hiyo kando kando ya vifusi vya Misikiti na majengo yaliyobomolewa na mabomu ya Wazayuni.

Image Caption

Baadhi ya nchi kama vile Saudi Arabia, Misri, Jordan, Palestina, Umoja wa Falme za Kiarabu, Tunisia, Algeria, na Libya zimetangaza leo Jumapili ya Julai 16 kuwa siku ya Idul al-Adh'ha.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Indonesia, Malaysia, Brunei, India na Oman pamoja na nchi kadhaa za Afrika zikiwemo Morocco na Mauritania zimetangaza kuwa, kwa kutegemea mwandamo wa mwezi, Jumatatu ya kesho Juni 17 itakuwa ni sikukuu ya Idul Adh'ha.

 

Tags