Jun 17, 2024 10:50 UTC
  • Baraza la mawaziri la vita la Israel lasambaratika

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimetangaza kuwa, Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala huo amelivunja baraza la mawaziri la vita la Israel.

Ripoti hiyo imesema kuwa, Netanyahu amelivunja baraza la mawaziri la vita kutokana na mizozo na ugomvi mkubwa uliowakumba viongozi wa utawala wa Kizayuni kuhusu kuendelea vita vya Ghaza, kusimamishwa vita na mabadilishano ya mateka.

Hayo yametangazwa leo Jumatatu na shirika la redio na televisheni la utawala wa Kizayuni ambalo limesema kuwa, Itamar Ben-Gvir, waziri wa usalama wa ndani wa utawala wa Kizayuni mwenye misimamo mikali kupindukia ya Kizayuni ametaka aingizwe kwenye baraza la mawaziri la vita, lakini Netanyahu ameamua kulivunja baraza hilo. 

Kanali ya 12 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni imetangaza kuwa, Netanyahu ameamua kuunda baraza dogo la mawaziri la kumshauri katika masuala nyeti zaidi ndio maana amelivunja baraza la mawaziri la vita.

Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth nalo limetangaza kuwa, Netanyahu ataunda baraza dogo la kisiasa ambalo litakuwa na waziri wa vita, waziri wa masuala ya kiistratijia pamoja na mkuu wa baraza la usalama wa ndani.

Kabla ya hapo pia Benny Gantz alikuwa amejitoa kwenye baraza la mawaziri la vita la Netanyahu na kumtaka waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni aitishe uchaguzi haraka sana. Vile vile alitaka waziri wa vita wa utawala huo atimuliwe kwenye baraza hilo.