Jun 18, 2024 07:09 UTC
  • Kusambaratika kwa Baraza la Mawaziri la Vita la Kizayuni

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amevunja Baraza la Mawaziri la Vita la utawala huo.

Kufuatia ombi la Itamar Ben-Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala haramu wa Israel la kutaka kujiunga na Baraza la Vita la utawala huo, Netanyahu amechukua uamuzi wa kulivunjilia mbali baraza hilo. Baraza hilo la vita limevunjwa pia baada ya Benny Gantz na Gadi Eisenkot, wajumbe wa zamani wa Baraza la Mawaziri la Vita la Kizayuni, kujiuzulu rasmi wakipinga utendaji wa Netanyahu, na kutaka uchaguzi wa mapema ufanyike.

Benjamin Netanyahu, alidhani kwamba vita vya Ukanda wa Gaza vingeleta umoja wa kisiasa kwenye utawala huo na ndio maana akaamua kuunda baraza la mawaziri la vita.

Lakini Benny Gantz, waziri wa zamani wa vita wa utawala wa Kizayuni, alitangaza kuwa kuwepo kwake katika baraza hilo kulitokana na hatima yao ya pamoja na sio ushirikiano wa kisiasa.

Ali Sharifinia, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: "Kujiuzulu kwa wajumbe wawili wa baraza la mawaziri la vita la Kizayuni kulitoa fursa kwa watu wenye misimamo mikali kama vile Itamar Ben Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Utawala wa Kizayuni, kujaribu kupenya na kuingia kwenye baraza hilo. Kwa hiyo inaonekana kwamba Netanyahu amechukua uamuzi wa kulivunja baraza la vita ili kuzuia mashinikizo ya kisiasa ya watu hao wenye misimamo mikali, ya kujaribu kujiunga na baraza la mawaziri la vita.

Duru za usalama za utawala wa Kizayuni, ambazo zina mitazamo sawa na ya Benny Gantz na Eisenkot, wajumbe wawili waliojiuzulu katika baraza la vita, kuhusu vita vya Ukanda wa Gaza, zimekuwa na wasiwasi kwamba kwa kujiuzulu wawili hao, Netanyahu na Ben Gvir wangekuwa waamuzi wakuu wa mambo katika baraza hilo.

Netanyahu anakabiliwa na kesi ya jinai za kivita katika mahakama ya ICC

Hii ni kwa sababu Ben Gvir, alikuwa amechukua hatua muhimu za kujiunga na baraza la mawaziri la vita, jambo ambalo bila shaka lingeibua wasiwasi mkubwa kuhusu matokeo ya uingiliaji wake katika vita vya Ukanda wa Gaza. Huku ikiwa imepita miezi minane tangu kuanza uvamizi wa utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza bila ya matokeo na mafanikio yoyote kwa watawala wa Tel Aviv, utawala huo unazidi kuzama katika kinamasi cha migogoro yake ya ndani na ya nje.

Katika kipindi hiki chote, utawala wa Kizayuni haujapata mafanikio yoyote zaidi ya kutekeleza mauaji ya umati dhidi ya watu wasio na hatia, kuharibu miundomsingi, kufanya jinai za kivita, ukiukwaji wa sheria za kimataifa, mashambulizi dhidi ya mashirika ya misaada na kusababisha njaa ya makusudi huko Ukanda wa Gaza. Utawala huo, haujaweza kufikia malengo yoyote uliyoyatangaza awali, yakiwemo ya kuwakomboa mateka wake na kuiangamiza Hamas, hata baada ya kufanya operesheni ya kijeshi na mauji ya kivita huko katika mji wa  Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Kwa hiyo Netanyahu anajiona kuwa mshindwa mkuu wa vita vya Gaza, na anafahamu vyema pia ukweli kwamba baada ya kumalizika vita hivyo, wapinzani wake watafanya juhudi za kumfikisha mahakamani kutokana na kesi chungu nzima za ufisadi zinazomkabili.

Kwa sababu hiyo, Benjamini Netanyahu ametangaza kwamba ataendeleza vita hadi atakapoiangamiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, na hii ni katika hali ambayo anajua vyema kwamba lengo hilo haliwezi kufikiwa kamwe.

Vyovyote vile itakavyokuwa, ni wazi kuwa Netanyahu anaendelea kufanya jinai anazozifanya huko Ukanda wa Gaza na kuendelea na maisha yake ya kisiasa katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) kwa ushirikiano na uungaji mkono kamili wa Marekani. Ni kwa kuzingatia ushirikiano na kushiriki huko kwa Joe Biden katika jinai za Netanyahu ndipo rais huyo wa Marekani akawa anakabiliwa na maandamano na malalamiko ya kila siku ya raia wa Marekani.