Ansarullah: Operesheni za Yemen zinaashiria kuimarika kambi ya muqawama
(last modified Fri, 21 Jun 2024 07:39:06 GMT )
Jun 21, 2024 07:39 UTC
  • Ansarullah: Operesheni za Yemen zinaashiria kuimarika kambi ya muqawama

Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema operesheni za nchi hiyo dhidi ya utawala haramu wa Israel ni ushahidi wa kupata nguvu na kuwa na umoja mrengo wa muqawama katika eneo la Asia Magharibi katika kuitetea Palestina.

Mohammed Abdul-Salam alisema hayo jana Alkhamisi katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon na kuongeza kuwa, "Operesheni hizo zinaonyesha kuwa kuna kambi halisi ya muqawama ambayo inazungumza na kuchukua hatua, na ni mrengo wa kweli ambao unanyanyuka na kufanya harakati panapohitajika."

Amesema moja ya matunda ya operesheni za vikosi vya Yemen dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na waungaji mkono wake ni kuondoa mivutano ya kimadhehebu katika nchi hiyo ya Kiarabu. 

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Ansarullah ameeleza bayana kuwa, "Msimamo wa Wayemen umelipa maana halisi suala la kuipa kipaumbele kadhia ya Palestina, pamoja na hali zetu ngumu."

Ansarullah inavyoshambulia meli za maadui Bahari Nyekundu

Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, na ikiwa ni katika kuwaunga mkono Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, jeshi la Yemen limejiunga kwenye kuwaunga mkono kivitendo Wapalestina hao, na harakati ya Kiislamu ya Ansarullah imekuwa ikizipiga meli za utawala wa Kizayuni wa Israel au meli yoyote inayoelekea kwenye bandari za utawala huo ghasibu kupitia Bahari Nyekundu.

Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameongeza kuwa, vikosi vya Yemen vitaendelea kuzishambulia meli za utawala huo au zile zinazoelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kupitia Bahari Nyekundu, hadi pale utawala wa Kizayuni utakaposimamisha mauaji ya umati na mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya Wapalestina wasio na hatia huko Gaza.