Jun 21, 2024 12:20 UTC
  • Armenia yalitambua rasmi taifa huru la Palestina

Serikali ya Armenia imetangaza kuwa, imelitambua rasmi taifa huru la Palestina.

Kwa tangazo hilo Armenia inakuwa nchi ya karibuni kabisa kutangaza kulitambua rasmi taifa huru la Palestina.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Armenia imetangaza hii leo kwamba, inalitambua rasmi taifa huru la Palestina, na hivyo kukaidi matakwa ya utawala haramu wa Israel ambao unapingana na hatua kama hizo.

Armenia imesisitiza kuwa, inaunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa la kusitisha mara moja mapigano katika Ukanda wa Gaza, pamoja na suluhisho la mataifa mawili katika mzozo wa Palestina na Israel.

"Ikithibitisha utiifu wake kwa sheria za kimataifa na kanuni za usawa, uhuru na kuishi pamoja kwa amani, Jamhuri ya Armenia inatambua taifa la Palestina," wizara hiyo imesema katika taarifa yake, ikisisitiza kwamba "Yerevan inataka kwa dhati ujio wa amani ya kudumu" katika kanda hii.

 

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Mei Uhispania, Ireland na Norway zilipasisha rasmi mpango wa kutambua rasmi Palestina, katika uamuzi ulioratibiwa hatua ambayo imeongeza himaya na uungaji mkono kwa Palestina barani Ulaya.

Makundi ya Muqawama ya Palestina yametoa mjibizo kwa utayarifu uliotangazwa na nchi kadhaa za Ulaya wa kuitambua nchi huru ya Palestina kwa kueleza kwamba hatua hiyo ni mabadiliko makubwa katika msimamo wa nchi mbalimbali duniani katika kuunga mkono piganio tukufu la taifa la Palestina.

Nchi za Ulaya zimekuwa zikifanya juhudi za kuitambua Palestina sambamba na kuongezeka idadi ya Wapalestina wanaouawa shahidi na wanaojeruhiwa katika Ukanda wa Ghaza kutokana na mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni.