Jun 23, 2024 02:47 UTC
  • Jenerali Mzayuni: Kutangaza vita na Hizbullah ni kujiua kwa umati Israel

Jenerali mmoja mstaafu wa jeshi la utawala wa Kizayuni ameonya vikali kuhusu kutangaza vita dhidi ya Hizbullah ya Lebanon na amekichukulia kitendo hicho kuwa ni kujiangamiza kwa umati utawala huo.

Jenerali Itzhak Brik ameandika makala iliyochapishwa katika gazeti la Kizayuni la Maariv kwamba, viongozi wa kijeshi na kisiasa wa Israel ambao tarehe 7 Oktoba waliruhusu kutokea maafa makubwa kwa kushindwa kutabiri na kuzuia operesheni ya HAMAS ya Kimbunga cha al Aqsa na wanaendelea kushindwa hadi leo hii, wanajiandaa kwa maafa mengine makubwa zaidi ya kutaka kuingia vitani na Hizbullah.

Aidha ameandika: "Wakati huu, kosa lao (maafisa wa kijeshi na kisiasa wa utawala wa Kizayuni) litakuwa baya zaidi kwa mamia ya maelfu ya watu iwapo wataanzisha vita vya kikanda dhidi ya Israeli."

 

Jenerali huyo Mzayuni amesema pia katika makala yake hiyo kwamba: “Mpango uliowasilishwa na mkuu wa majeshi, Herzi Halevi, na Yoav Galant, waziri wa vita wa Israel wa kuanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Hizbullah ya Lebanon kwa njia ya nchi kavu, anga na baharini, pendekezo ambalo limekubaliwa pia na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu utapelekea Israel kushambuliwa kutoka pande sita na kila siku maelfu ya makombora, maroketi na ndege zisizo na rubani zitamiminika ndani la Israel.

Amesema, kwa maneno machache napenda kusisitiza kuwa, mpango mpango huo ni kujiangamiza kwa umati Israel inayoongozwa na watu hawa watatu (Netanyahu, Gallant na Halevi). Hawana chochote cha kupoteza, ndio maana wanachezea hatima ya Israel na lengo lao ni kuipeleka kuzimu.

Jenerali huyo mstaafu wa jeshi la Israel amekumbusha tena kwa kusema: "Ni makamanda hawa hawa ndio ambao wameshindwa kuiangamiza Hamas katika eneo dogo mno la Ukanda wa Ghaza, leo wanataka kulipeleka jeshi la Israel kwenye vita vikubwa zaidi. Afisa huyo wa ngazi za juu wa jeshi la Israel aidha amesema: "Jeshi letu dogo haliwezi kushinda hata upande mmoja."