Saudia yakanusha kuhusika na shambulio la Israel Hudaydah; Iran yalaani
(last modified Sun, 21 Jul 2024 06:50:09 GMT )
Jul 21, 2024 06:50 UTC
  • Saudia yakanusha kuhusika na shambulio la Israel Hudaydah; Iran yalaani

Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia imekadhibisha ripoti za vyombo vya habari vya Israel kuwa Riyadh imeshiriki katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya mji wa al-Hudaydah, magharibi mwa Yemen.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Saudia, Brigedia Jenerali Turki al-Maliki amesema, Riyadh haijahusika kivyovyote katika hujuma hizo za anga zilizofanywa na ndege za kivita za Israel dhidi ya mji wa al-Hudaydah jana Jumamosi.

Brigedia Jenerali Turki al-Maliki ameongeza kuwa, Saudi Arabia haitauruhusu upande wowote uhujumu anga yake. Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree ameyataja mashambulizi hayo ya anga kuwa ni "uchokozi mbaya" ambao umelenga miundo mbinu ya kiraia.

Saree amesisitiza kwamba, vikosi vya jeshi la Yemen "vimejiandaa kwa vita vya muda mrefu na adui huyu hadi uchokozi dhidi ya Gaza utakapokoma, mzingiro uondolewe, na uhalifu wote unaofanywa dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza ukomeshwe."

Katika hatua nyingine, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran sanjari na kulaani mashambulizi hayo ya anga yaliyofanywa na ndege za kivita za Israel katika mji wa al-Hudaydah, magharibi mwa Yemen, amesema Wayemen wanalipa gharama kwa kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Nasser Kan'ani amesema mashambulio hayo ya Wazayuni dhidi ya mji huo wa bandari wa Yemen yanaonesha hulka ya unyama na ukatili ya utawala huo pandiziki.

Amesisitiza kuwa, mauaji ya watu wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza ndio mzizi wa taharuki na mivutano inayoshuhudiwa katika eneo la Asia Magharibi.

Tags