Oct 06, 2024 11:55 UTC
  • Wapalestina 24 wauliwa shahidi katika mashambulizi ya Israel katikati mwa Gaza

Wapalestina 24 wameuawa shahidi na 94 kujeruhiwa katika jinai za leo za jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Televisheni ya al Jazeera imetangaza kuwa jeshi la utawala wa Israel leo asubuhi limewashambulia wakimbizi wa Kipalestina katika msikiti mmoja karibuni na Hospitali ya Mashahidi wa al Aqsa katika mji wa Deir al Balah katikati mwa Gaza na kuwauwa shahidi raia 24 wa Kipalestina na kujeruhi wengine 94.  

Jinai za Israel za kubomoa kambi ya wakimbizi Ukanda wa Gaza

Watu wengine kadhaa pia wamejeruhiwa katika shambulio la jeshi la Israel katika shule ya wakimbizi wa Kipalestina katika eneo la al-Zawaida katikati mwa Ukanda wa Gaza. 

Jeshi la utawala wa Kizayuni linaendelea kuficha jinai zake kwa visingizio visivyo na msingi na kudai kuwa, wapiganaji wa harakati ya Hamas ndio walioshambulia shule ya Ibn Rushd na Msikiti wa Mashahidi wa al Aqsa katika eneo la Deir al Balah. 

Habari nyingine zinasema kuwa, "Hassan Hamad", mwandishi wa habari wa Kipalestina ameuawa shahidi asubuhi ya leo katika shambulio la jeshi la Israel kwenye nyumba yake katika kambi ya Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. 

Kwa kuuawa shahidi mwana habari huyo, idadi ya  waandishi habari waliouliwa shahidi na Israel tangu kuanza mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza mwezi Oktoba imefikia 175.