Uingereza yakiri, Hizbullah ina nafasi chanya nchini Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i11935-uingereza_yakiri_hizbullah_ina_nafasi_chanya_nchini_lebanon
Balozi wa Uingereza mjini Bairut amesema kuwa, ni jambo lisilofaa kuilaumu harakati ya Hizbullah ya Lebanon kwa kushiriki katika vita dhidi ya wapiganaji wa kundi la Daesh nchini Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 25, 2016 00:22 UTC
  • Uingereza yakiri, Hizbullah ina nafasi chanya nchini Lebanon

Balozi wa Uingereza mjini Bairut amesema kuwa, ni jambo lisilofaa kuilaumu harakati ya Hizbullah ya Lebanon kwa kushiriki katika vita dhidi ya wapiganaji wa kundi la Daesh nchini Syria.

Hugo Shorter, amesisitiza kuwa, kutokana na hatari ya uepo wa wanachama wa Daesh kwa Lebanon, ni suala la kawaida kwa harakati hiyo ya Hizbullah kushiriki vita dhidi ya magaidi hao nchini Syria. Akiashiria kwamba kundi la Daesh limeenea katika nchi zote za dunia na si katika Mashariki ya Kati pekee, Shorter ameongeza kuwa, Uingereza ina imani na vyombo vya usalama vya Lebanon na jeshi la nchi hiyo.

Wanamapambano wa harakati ya Hizbullah

Kukiri kwa balozi huyo juu ya nafasi chanya ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon katika kupambana na ugaidi na mchango wake mzuri nchini humo, kumejitokeza katika hali ambayo, kabla ya hapo pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa alifanya safari nchini Lebanon na kukutana na viongozi wa serikali na pia viongozi wa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah, suala ambalo lilikabiliwa na upinzani mkali na vitisho kutoka kwa utawala haramu wa Israel. Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala huo ghasibu ilikosoa vikali safari hiyo ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa nchini Lebanon na kukutana kwake na viongozi wa Hizbullah. Kuhusiana na suala hilo, gazeti la Lebanon la al-Jamhuriyyah liliandika kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa ilikuwa imeomba kukutana na Mohammad Raad, kiongozi wa mrengo wenye mfungamano na harakati hiyo, hata hivyo Hizbullah ilikataa ombi hilo na badala yake ikaridhia Ali Fayyadh, mwakilishi wa Hizbullah katika Bunge la nchi hiyo na Ammar Musawi, mkuu wa Ofisi ya Mahusiano ya Kimataifa ya Hizbullah wakutana na Waziri huyo Ufaransa.

Wanamapambano wa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah wakiwa katika maonyesho ya kijeshi

Sisitizo la Ufaransa la kutaka kukutana na viongozi wa Hizbullah ya Lebanon licha ya kuwepo pingamizi kubwa la utawala wa Kizayuni, limekuja huku duru za habari za nchi za Ulaya zikiripoti azma ya viongozi wa nchi hizo ya kutaka  kushirikiana na harakati hiyo ambayo ina nafasi kubwa na yenye taathira chanya kutokana na kupendwa kwake na raia wa Lebanon na wa eneo zima la Mashariki ya Kati. Katika fremu hiyo kiongozi wa Waislamu wa Kisuni nchini Lebanon ametangaza kuwa, kuugusa kwa aina yoyote muqawama wa Lebanon, ni sawa na kulifanyia usaliti taifa la Lebanon.

Wanamapambano wa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah wakiwa katika maonyesho ya kijeshi

Sheikh Mahir Abdul-Razzaq kiongozi wa kiroho wa Waislamu wa Kisuni na mkuu wa Harakati ya Marekebisho na Umoja wa Lebanon, aliyasema hayo katika mkutano wa maadhimisho ya kumbukumbu ya ushindi wa Hizbullah hapo mwezi Julai mwaka 2006 na kuongeza kuwa, wadhifa wa kisheria na kitaifa wa Walebanon ni kuunga mkono muqawama na kwamba, kuugusa kwa aina yoyote na silaha zake ni usaliti dhidi taifa na wananchi wa Lebanon. Aliongeza kuwa, kitendo hicho ni kuutumikia utawala haramu wa Israel, makundi ya kitakfiri na kigaidi na ni dhidi ya Lebanon na ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu kwa ujumla. 

Raia wa Lebanon wakionyesha uungaji mkono wao kwa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah

Sheikh Mahir Abdul-Razzaq amewataka raia wa Lebanon kuiunga mkono harakati hiyo na jeshi la serikali na kusisitiza kuwa, muqawama na jeshi ndio mstari wa mbele wa ulinzi wa Lebanon dhidi ya maadui katika kulinda usalama wa nchi. Aliongeza kuwa, mihimili hiyo miwili na kujitolea kwao kukubwa, imeweza kuushinda utawala wa Kizayuni na makundi ya kitakfiri na kigaidi.

Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa harakati hiyo ya Hizbullah ya Lebanon

Naye Suleiman Frangieh, kiongozi wa harakati ya Marada ya Lebanon ametangaza uungaji wake mkono kwa harakati ya Hizbullah kutokana na juhudi zake za kudhamini usalama wa nchi hiyo. Frangieh pia amewataka raia wa nchi hiyo kumuunga mkono Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa harakati hiyo ya Hizbullah ya Lebanon katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel.