Ripota Maalumu wa UN: Poland inapaswa kumkamata Netanyahu
(last modified Sat, 11 Jan 2025 06:42:14 GMT )
Jan 11, 2025 06:42 UTC
  • Francesca Albanese
    Francesca Albanese

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Francesca Albanese ametoa wito wa kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, iwapo atazuru Poland, na kusema kuwa Warsaw lazima ifuate kanuni za haki za kimataifa.

Francesca Albanese alisema jana Ijumaa kuwa wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wanatakiwa kuwakamata watu ambao mahakama hiyo imetoa hati za kukamatwa kwao, na kuongeza kuwa: "Poland, ambayo ililaani kushindwa kwa Mongolia kumkamata Rais wa Russia, Vladimir Putin, inapaswa kumkamata Netanyahu, kwa sababu ubaguzi katika utekelezaji wa sheria unadhoofisha mfumo wa haki wa kimataifa."

Wakati huo wananchi wa Poland walifanya maandamano jana huko Warsaw wakipinga uamuzi wa serikali ya nchi hiyo kumpa kinga Netanyahu na kuzuia kukamatwa kwake.

Itakumbukwa kuwa, Novemba 21, 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu yenye makao yake The Hague huko Uholanzi ilitoa kibali cha kutiwa nguvuni Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na aliyekuwa waziri wake wa vita, Yoav Gallant kwa tuhuma za kutenda jinai za kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Ukanda wa Gaza.