"Bila kudhibitiwa Uwahabi, ugaidi hautokuwa na mwisho duniani"
Mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Iraq amesema, bila kudhibitiwa Uwahabi, ugaidi hautotokomezwa duniani.
Muwaffaq al-Rubai'i amesema, bila ya jamii ya kimataifa kulidhibiti tapo potofu na chafu la Uwahabi hakuwezi kuwepo na matumaini ya kushuhudia mwisho wa ugaidi duniani.
Al-Rubai'i amesisitiza kuwa: ni kosa kubwa kudhani kwamba ugaidi unatokana na migogoro ya kiusalama, kisiasa na kiuchumi; ugaidi chimbuko lake ni pote potofu na chafu la Uwahabi.
Mbunge huyo wa bunge la Iraq amefafanua kuwa Boko Haram, Al-Qaeda, wahusika wa matukio ya Septemba 11, Daesh, Jabhatu-Nusra na magenge mengine yote ya kigaidi duniani yamesibiwa na kirusi cha Uwahabi ambacho kimeziharibu bongo za baadhi ya watu.
Mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Iraq aidha ametahadharisha kuwa ugaidi utayakumba maeneo mapya katika mabara ya Ulaya, Asia na Afrika na utatumia mbinu mpya za kigaidi ambazo zinaweza zisiwe za kutumia silaha na mada za miripuko zilizozoeleka; bali yamkini ukatumia silaha za maangamizi na mbinu mpya za mauaji.../