Nchi za Kiarabu zapinga kuhamishwa Wapalestina wa Gaza
Nchi kubwa za Kiarabu zimepinga pendekezo la Rais wa Marekani, Donald Trump, la kuwafukuza Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza na kuwapeleka nje ya nchi yao.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi tano za Kiarabu wametoa taarifa ya pamoja ya kupinga mpango huo wa kuwalazimisha Wapalestina kuhama kutoka katika ardhi yao. Mawaziri wa Mambo ya Nje na maafisa kutoka Misri, Jordan, Saudi Arabia, Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu, Mamlaka Ndani ya Palestina na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wamesema pendekezo hilo la Trump linatishia uthabiti katika eneo, kueneza migogoro na kudhoofisha misingi ya amani.
Sehemu moja ya taarifa hiyo inasema, "Tunapinga [jaribio lolote] la kuhatarisha haki za Wapalestina zisizopingika, iwe kupitia ujenzi wa vitongoji vya walowezi, au kufukuzwa (Wapalestina), au kuunganishwa ardhi (na ardhi za Palestina zilizoghusubiwa), au kwa kupokonywa ardhi kutoka kwa wamiliki wake, kwa namna yoyote au kwa hali yoyote, au kuhalalisha kivyovyote."
Mkutano huo umefanyika baada ya Trump kusema wiki iliyopita kwamba, Misri na Jordan zinapaswa kuwachukua Wapalestina kutoka Gaza, eneo aliloliita "mahali pa uharibifu" kufuatia miezi 15 ya mashambulizi ya Israel ambayo yamewafanya wengi wa wakazi wake milioni 2.3 kukosa makazi.
Mpango huo wa Trump umeendelea kukabiliwa na upinzani mkubwa wa jamii ya kimataifa. Raia wa Misri walikusanyika Ijumaa mbele ya kivuko cha mpakani cha Rafah na Ukanda wa Gaza wakipinga pendekezo hilo la Trump, la kuwafukuza Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza na kuwapeleka nje ya nchi yao.
Mnamo Januari 25, Trump alipendekeza kuwahamisha Wapalestina wa Ukanda wa Gaza na kuwapeleka katika nchi jirani kama vile Misri na Jordan, kwa kisingizio cha "ukosefu wa maeneo ya kuishi katika eneo hilo lililoharibiwa na Israel kwa kutumia silaha za Marekani yenyewe katika kipindi cha zaidi ya miezi 15.