Arab League yapinga njama za Trump za kuipora Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i122376-arab_league_yapinga_njama_za_trump_za_kuipora_ghaza
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League), imepinga njama mpya za rais wa Marekani, Donald Trump za kutaka kuipora Ghaza na kuwaondoa Wapalestina kwenye eneo lao hilo. Arab League imesema, mpango huo wa Trump ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
(last modified 2025-02-06T06:55:28+00:00 )
Feb 06, 2025 06:55 UTC
  • Arab League yapinga njama za Trump za kuipora Ghaza

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League), imepinga njama mpya za rais wa Marekani, Donald Trump za kutaka kuipora Ghaza na kuwaondoa Wapalestina kwenye eneo lao hilo. Arab League imesema, mpango huo wa Trump ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Jumanne usiku, Trump alitumia kisingizio cha kuweko uharibifu mkubwa uliosababishwa na mashambulizi ya kikatili ya jeshi la Israel kama ujanja wa kuondolewa kabisa Wapalestina kwenye Ukanda wa Ghaza na kupelekwa nchi jirani za Kiarabu. Alisema anataka Ghaza iwe ni milki ya Marekani. 

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imejibu njama hizo kupitia taarifa rasmi na kusema: "Bila ya shaka, nchi zote za Kiarabu zina kauli moja kuhusu misingi ya kadhia ya Palestina, na moja ya msingi muhimu zaidi ni kupatikana haki halali za Wapalestina za kuwa na nchi yao huru mji mkuu wake ukiwa ni Baytul Muqaddas Mashariki."

Taarifa hiyo inasema: "Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza ni maeneo ya taifa la baadaye la Palestina. Kwa hivyo, mpango wa Trump na njama za kuendelea kuwahamisha Wapalestina na kuwapeleka nje ya maeneo yao haukubaliki na unakiuka sheria za kimataifa. Mpango huu ni kichocheo cha ukosefu wa utulivu na hausaidii yoyote katika jitihada za kuleta amani na usalama katika eneo hili."

Kwa upande wake, Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza wameubeza na kuukebehi mpango wa rais wa Marekani wa kuwataka wahame moja kwa moja katika ardhi yao hiyo ya Palestina ili kupisha ujenzi wa kuigeuza Ghaza eneo la burudani watakaloishi ndani yake watu wa kila pembe ya dunia. Kufuatia kauli ya Donald Trump kwamba Marekani italitwaa na kulimiliki eneo la Ghaza, Wapalestina wa eneo hilo wametoa mijibizo wakisisitiza kuwa wataishi au kufia katika ardhi yao hiyo.