Misri: Amani haitapatikana pasi na kuundwa nchi huru ya Palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema kuwa, hakutakuwa na usalama katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) bila ya kuasisiwa taifa la Palestina.
Badr Abdelatty amesema hayo na kuashiria kuwa Cairo inashirikiana na pande za Marekani na Qatar ili kuhakikisha kunapatikana uthabiti wa usitishaji vita na kuanza kwa awamu ya pili ya mazungumzo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdel Ati alisema: Tunazitegemea nchi za Umoja wa Ulaya kufanya juhudi zaidi za kuleta utulivu wa usitishaji vita huko Gaza na kuufanya kuwa endelevu.
Abdul Ati amesisitiza ulazima wa kujaribu kuujenga upya Ukanda wa Gaza bila ya kuwatimua Wapalestina na kusema: Hakuna mbadala wa UNRWA (Shirika la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina) na nafasi yake katika Ukanda wa Gaza na ardhi za Wapalestina.
Abdul Ati ameongeza kuwa: Bila ya kuundwa taifa la Palestina, hakutakuwa na usalama kamwe katika eneo la Asia Magharibi, na tunajaribu kupata uungaji mkono wa kimataifa kwa mpango wa kujenga upya Ukanda wa Gaza, kama ambavyo Misri inaendeleza juhudi zake za kuanza awamu ya pili ya mazungumzo ya kusitisha mapigano huko Gaza.
Mwanadiplomasia huyo wa Misri ameongeza kuwa: Hakuna mbadala wa kufuatwa kikamilifu na kwa uaminifu kwa vipengee vyote vya makubaliano ya usitishaji vita na kubadilishana wafungwa huko Gaza. Aidha amesema, mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu watafanya mkutano nchini Saudi Arabia baada ya mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.