Misri, Saudia zalaani Israel kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza
(last modified Mon, 03 Mar 2025 07:07:43 GMT )
Mar 03, 2025 07:07 UTC
  • Misri, Saudia zalaani Israel kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza

Hatua ya Israel ya kuzuia kuingizwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza imelaaniwa na Misri na Saudi Arabia, huku nchi mbili hizo zikisisitiza kuwa kitendo hicho ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Wizara za Mambo ya Nje za Saudi Arabia na Misri zilitoa taarifa tofauti jana Jumapili baada ya Israel kusitisha msaada wa kibinadamu katika eneo hilo lililozingirwa la Palestina, ili kuishinikiza Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hamas kukubali pendekezo lililotolewa na Marekani la kuongeza muda wa awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo ilimalizika juzi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Sama la Palestina, Misri, ambayo pamoja na Marekani na Qatar imekuwa mpatanishi wa makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza, ilisema kuwa hatua ya Israel ya kuzuia misaada ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano na sheria za kimataifa za kibinadamu.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia pia imelaani hatua ya Israel ya kuzuia misaada ya kibinadamu huko Gaza, na kueelza kuwa inatumia suala hilo kama chombo cha uporaji na adhabu ya jumla.

Shirika rasmi la Habari la Saudi (SPA) limeripoti kuwa: Kitendo hiki, wizara ilisema, ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na ukiukaji wa moja kwa moja wa kanuni na sheria za kimataifa za kibinadamu. 

Riyadh kwa mara nyingine tena imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuzuia vitendo hivi, kuanzisha mchakato wa kimataifa wa uwajibikaji, na kuhakikisha kwamba Wapalestina huko Gaza wanapata misaada endelevu.

Kabla ya hapo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ililaani pia uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza na kuonya juu ya madhara ya hatari ya hatua hiyo katika mgogoro wa sasa hususan katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.