Hamas: Taifa la Palestina litajitawala lenyewe katika ardhi yake
Mmoja wa viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema: "Gaza" na "Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni mali ya wenyeji wa maeneo hayo.
Khalid Mash'al ambaye ni miongoni mwa viongozi wa harakati ya muqawama ya Hamas amesisitiza kuwa: Gaza na Ukingo wa Magharibi ni mali ya Wapalestina na kwamba hatua zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni si tu kuwa zinatishia Gaza na Ukingo wa Magharibi bali hata nchi nyingine za kanda hii.
Mash'al amesisitiza kuwa: Wananchi wa Palestina wenyewe ndio watakaoendesha masuala ya nchi yao na kutawala ardhi hiyo na wanapinga jitihada zozote za kuasisi mfumo wa kisiasa kutoka nje au kuupokonywa silaha muqawama chini ya usimamizi wa Wazayuni maghasibu.
Mwakilishi huyo wa ngazi ya juu wa Hamas amesema, muqawama hautaweka chini silaha zake madhali maghasibu Wazayuni bado wangalipo katika ardhi za Palestina na mapambano ya silaha ni njia pekee ya kupigania haki za Palestina zilizoporwa.
Khalid Mash'al ametahadharisha kuwa Gaza inakabiliwa na hatari kubwa; ikiwa ni pamoja na njama za kuwasababishia njaa wakazi wa eneo hilo kwa lengo la kuwafukuza kwa nguvu.
Kuhusu hali ya ndani ya Palestina, Mash'al amesisitiza kuwa umoja wa safu za Wapalestina ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zilizopo.