Makumi ya wanawake, watoto wauawa na mabomu ya Wazayuni Gaza
Mashambulizi makali ya anga ya utawala wa Kizayuni wa Israel yameua shahidi zaidi ya Wapalestina 20, wakiwemo wanawake na watoto wadogo katika Ukanda wa Gaza.
Press TV imeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, shambulizi la anga la mapema alfajiri lililolenga nyumba moja katika kitongoji cha Al-Tuffa katika mji wa Gaza leo Jumatano limeua shahidi watu 10.
"Timu zetu zilihamisha mashahidi 10 na majeruhi kadhaa hadi katika Hospitali ya al-Shifa baada ya nyumba ya familia ya Hassouneh kushambuliwa," Msemaji wa Shirika la Ulinzi wa Raia, Mahmud Bassal amesema.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Ma'an la Palestina, mashambulizi ya Israel mapema leo Jumatano "yalilenga zaidi mji wa Gaza" na kusababisha vifo vya takriban watu 21 na makumi ya wengine kujeruhiwa.
Watu watatu wa familia moja walipoteza maisha kutokana na shambulio la makombora dhidi ya Wapalestina waliokuwa wamekimbia makazi yao na kuishi kwenye mahema katika uwanja wa Yarmouk katikati mwa jiji hilo.
Jeshi katili la utawala haramu wa Israel lilianzisha tena mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza mnamo Machi 18, na tangu wakati huo limewaua watu 1,650 na kuwajeruhi zaidi ya 4,300; baada ya kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano na kubadilishana wafungwa yaliyofikiwa Januari.
Mashambulizi hayo mapya ya anga ya utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza yamefanya idadi ya vifo kutokana na vita vya kinyama vya Israel vilivyoanza Oktoba, 2023 kupindukia 51,000.