HAMAS yakataa pendekezo la kuweka silaha chini
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeripotiwa kupinga pendekezo la utawala haramu wa Israel la kusitisha vita kwa muda wa wiki sita katika Ukanda Gaza, sambamba na kulitaka kundi hilo la muqawama kuafiki kupokonywa silaha.
Hii inaaminika kuwa ni mara ya kwanza kwa Israel kuipa HAMAS sharti la kupokonywa silaha mkabala wa kusitisha mapigano, na hivyo kuashiria mabadiliko makubwa katika msimamo wake wa mazungumzo.
Akizungumza na shirika la habari la BBC, afisa mmoja wa Palestina ameishutumu Israel kwa kutumia mazungumzo hayo kukwamisha mambo, huku ikilenga kuwakomboa mateka.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alitangaza kuwa, eti atawaruhusu viongozi wa HAMAS kuondoka katika Ukanda wa Gaza iwapo harakati hiyo itakabidhi na kuweka chini silaha zake.
Hii ni katika hali ambayo, vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti leo Alkhamisi kuwa, ndege za kivita za Israel zimeshambulia kwa mabomu mahema kadhaa ya Wapalestina waliokimbia makazi yao katika eneo la kusini la Khan Younis, na kuua watu 23.
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa wito wa dharura kwa watu wa dunia kushiriki kikamilifu katika maandamano ya wiki moja ya kushinikiza kusitishwa kwa kampeni ya kutisha ya Israel ya mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza.
Katika taarifa ya Jumatano, HAMAS imetoa wito kwa "mataifa ya Kiarabu na Kiislamu na watu huru" wa dunia kushiriki maandamano hayo ya kimataifa katika siku za Ijumaa, Jumamosi, na Jumapili (Aprili 18, 19 na 20).