Iran yakataa madai ya kuhusika katika operesheni za kulipiza kisasi za Yemen
Iran imelaani vikali tuhuma za hivi karibuni zilizotolewa na maafisa wa Marekani na Israel kuhusu kuhusika kwake katika operesheni za kulipiza kisasi za Yemen, ikizitaja kuwa “hazina msingi” na “zinapotosha.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema Jumapili usiku kwamba uamuzi wa Yemen kuunga mkono watu wa Palestina ni uamuzi wa kujitegemea, unaotokana na ubinadamu wa taifa la Kiislamu na mshikamano wao na Wapalestina.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amebainisha kuwa ni jeshi la Marekani ndilo lililoingia vitani na Yemen kwa ajili ya kuunga mkono mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza.
Araghchi amekashifu Marekani kwa kutenda uhalifu wa kivita kwa kulenga miundombinu na maeneo ya kiraia katika miji mbalimbali ya Yemen.
Aliyaita madai hayo kuwa mbinu za kupotosha zenye lengo la kugeuza macho kutoka kwenye uhalifu unaofanywa na utawala wa Kizayuni katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu, kuficha kushindwa kwao kimkakati, na kutoa sababu ya kuendeleza hali ya machafuko katika eneo hilo.
Mwisho, Araghchi alilaani mashambulizi ya Marekani dhidi ya Yemen kama ukiukaji wa wazi wa Katiba ya Umoja wa Mataifa na kanuni za msingi za sheria za kimataifa.
Wakati huo huo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, pia alikataa vikali tuhuma hizo zisizo na msingi.
Baghaei alisema kwamba kuhusisha hatua za kishujaa za taifa la Yemen na Iran ni dharau kwa taifa hili lenye nguvu lakini pia linaloonewa.
Amesema kwamba uamuzi wa watu wa Yemen kuunga mkono Wapalestina ni uamuzi wa kujitegemea, unaotokana na ubinadamu wao na mshikamano wa Kiislamu na watu wa Palestina.
Amesisitiza kuwa ni jeshi la Marekani ndilo linalotekeleza uhalifu wa kivita kwa kuwashambulia watu wa Yemen na miundombinu ya kiraia kwa ajili ya kuunga mkono mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza.
Baghaei amebainisha kuwa kuhusisha operesheni za Yemen na Iran ni mbinu ya kugeuza macho kutoka kwenye uhalifu wa utawala wa Kizayuni nchini Palestina na kisingizio cha kupandikiza hali ya kutoaminiana na kutokuwa na usalama katika eneo la Asia Magharibi.
Pia amelaani vitisho vya hivi karibuni vilivyotolewa kwa Iran na Marekani na Israel, na kuiweka serikali ya Marekani na utawala wa kigaidi wa Kizayuni kuwa na jukumu la moja kwa moja kwa matokeo yake.
Vikosi vya Yemen vilisema Jumamosi kwamba vilikuwa vimefanya shambulizi la kombora la nne ndani ya saa 24 dhidi ya maeneo yanayokaliwa na Israel, na kusababisha kengele za tahadhari za mashambulizi ya anga kuwashwa katika maeneo kadhaa.