Maandamano makubwa Ufaransa kulaani kuongezeka kwa chuki dhidi ya Uislamu
Maelfu ya watu waliandamana katika mitaa ya Paris na miji mingine ya Ufaransa siku ya Jumapili kulaani ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu na kumuenzi Aboubakar Cissé, kijana kutoka Mali aliyeuawa akiswali ndani ya msikiti.
Maandamano hayo mjini Paris yalihudhuriwa na wanachama wa chama cha kisiasa cha mrengo wa kushoto cha La France Insoumise (LFI), wakiwemo Jean-Luc Mélenchon na wabunge kadhaa wa chama hicho. Waandamanaji walibeba mabango yenye jumbe kama vile, “Ubaguzi wa rangi huanza kwa maneno na kuishia kama ilivyomtokea Aboubakar.”
Tarek, meneja wa uzalishaji mwenye umri wa miaka 44 kutoka eneo la Paris, alisema, “Kifo cha Aboubakar Cissé ni kuvuka mstari mwekundu,” huku akiwa ameshika bendera kubwa ya Ufaransa.
Waandaaji wanaokadiriwa kuwa watu 15,000 walihudhuria maandamano ya Paris. Maandamano mengine pia yalifanyika katika miji ya Lille, Lyon na Marseille.
Mbunge wa LFI, Éric Coquerel, alisema, “Kuna ongezeko lisilopingika la chuki dhidi ya Uislamu, na mauaji ya Aboubakar Cissé ndani ya msikiti ni kilele cha hali hiyo.”
Alimkosoa Waziri wa Mambo ya Ndani, Bruno Retailleau, kwa kusema, “Hatutaacha kuwawajibisha wale wanaofuta mipaka kati ya siasa za mrengo wa kulia na zile za mrengo mkali wa kulia.” Alitoa hakikisho kwa Waislamu wa Ufaransa kwa kusema: “Hatutakata tamaa.”
Katika mji wa Marseille, bango moja lilisomeka: “Chuki dhidi ya Uislamu, huumiza, hubagua, hudhalilisha… Tosha.” Padri wa Kanisa Katoliki na mchungaji wa Kiprotestanti pia walihudhuria maandamano hayo, wakitoa wito wa kuishi kwa amani na kuheshimiana.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa iliripoti ongezeko la asilimia 72 la matukio ya chuki dhidi ya Waislamu katika miezi mitatu ya mwanzo wa mwaka huu, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita, ambapo visa 79 vilirekodiwa.
Mnamo Aprili 25, Aboubakar Cissé, kijana mwenye umri wa miaka 22, alichomwa kisu mara 57 hadi kufa ndani ya ukumbi wa kuswalia katika Msikiti wa Khadidja uliopo La Grand-Combe, mkoa wa Gard. Mshambuliaji anaripotiwa kurekodi tukio hilo huku akitamka matusi dhidi ya Uislamu. Mtuhumiwa tayari amefunguliwa mashtaka rasmi ya "mauaji ya kukusudia kwa misingi ya rangi au dini" na kwa sasa anashikiliwa rumande.