Milio ya risasi yasikika Tripoli baada ya mauaji ya kiongozi wa wanamgambo
(last modified Tue, 13 May 2025 07:03:32 GMT )
May 13, 2025 07:03 UTC
  • Milio ya risasi yasikika Tripoli baada ya mauaji ya kiongozi wa wanamgambo

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kukomeshwa haraka machafuko katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, huku watu wenye silaha wakifyatuliana risasi katika wilaya za kusini mwa mji huo baada ya mauaji ya kiongozi aliyekuwa na nguvu wa kundi moja la wanamgambo.

Wito huo wa mapema leo Jumanne umetolewa huku wakazi wa Tripoli wakiripoti kusikia milio ya risasi na milipuko katika vitongoji vingi kuanzia saa tisa alasiri ya jana Jumatatu.

Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar imeripoti kutoka Libya kwamba vyanzo vya usalama vimethibitisha kuuawa kwa Abdel Ghani al-Kikli, anayejulikana kama "Gheniwa", ambaye ni mkuu wa wanamgambo wenye nguvu wa Stability Support Authority (SSA).

Baada ya hapo, milio ya risasi na mapigano yaliripotiwa maeneo kadhaa ya Tripoli.

Al-Kikli alikuwa mmoja wa viongozi wa wanamgambo wenye ushawishi mkubwa katika mji mkuu wa Libya, Tripoli na hivi karibuni alihusika katika migogoro na makundi hasimu yenye silaha.

Ripoti zinasema takriban watu sita wamejeruhiwa, ingawa bado haijafahamika kama ni wanachama wa kikosi cha usalama au raia.

Katika taarifa yake iliyotolewa muda mfupi baada ya mapigano kuanza, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) umesema "umesikitishwa na hali ya usalama inayoendelea kuzorota huko Tripoli, na mapigano makali ya kutumia silaha nzito katika maeneo yenye wakazi wengi".

UNSMIL imeongeza kuwa "inatoa wito kwa pande zote kusitisha mapigano mara moja na kurejesha utulivu, na inakumbusha pande zote wajibu wao wa kulinda raia wakati wote".