Malengo ya safari ya Trump katika nchi tatu za Kiarabu
Rais Donald Trump wa Marekani alianza safari ya siku tatu katika nchi tatu za kusini mwa Ghuba ya Uajemi, Saudi Arabia, Imarati (UAE) na Qatar kuanzia Jumanne, Mei 13.
Kama ilivyokuwa katika muhula wa kwanza wa urais wake, Trump ameichagua Saudi Arabia kama kituo cha kwanza katika safari yake hiyo ya kwanza nje ya nchi. Washington imesema kuwa, lengo la safari hii ni kuimarisha ushirikiano wa kistratijia na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi. Awali vyombo vya habari vya Marekani viliripoti kuhusu safari ya Trump katika nchi za Ghuba ya Uajemi kwa kuzingatia matamshi ya maafisa wa sasa na wa zamani wa Marekani na maafisa wawili wa Kiarabu kwamba lengo lake ni kuhuisha makubaliano na ahadi za uwekezaji zenye thamani ya dola trilioni moja.
Safari ya Trump katika Ghuba ya Uajemi ambayo kwa mujibu wa Ikulu ya White House ina lengo la kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kiusalama na nchi za kusini wa Ghuba ya Uajemi, imeibua maswali mengi kuhusu mahusiano ya Marekani na nchi hizo, mahusiano ambayo yanaonekana kuwa yanalenga zaidi kuinufaisha Marekani kiuchumi na kibiashara kabla ya jambo jingine lolote. Kwa hakika, safari hii, ambayo Trump ameiita kuwa ya kihistoria na baadhi ya vyombo vya habari kukadiria faida zake za kiuchumi kwa Marekani kufikia dola trilioni 3, inalenga zaidi kudhamini maslahi ya kiuchumi ya upande mmoja, ambao ni Marekani.
Mtazamo wa Trump kuhusu nchi hizo uko wazi kutokana na matamshi yake ya huko nyuma kuhusu nchi za Kiarabu hususan Saudi Arabia. Trump amekariri mara kadhaa kauli yake ya kuifananisha Saudi Arabia na "ng'ombe wa kukamwa." Kauli hizi zenye utata sasa zinafasiriwa na baadhi ya wakosoaji kama ishara ya mtazamo wa udhalilishaji wa Marekani kuhusu nchi hizi. Shirika la habari la Axios limeripoti kwamba safari ya Trump huko Saudi Arabia, Qatar, na Umoja wa Falme za Kiarabu inahusiana zaidi na pesa kuliko jambo jingine lolote. Afisa mmoja wa Kiarabu amesema ajenda yake ya kikanda ni biashara, biashara na biashara.
Kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani, moja ya malengo makuu ya safari hii ni kuvutia uwekezaji mkubwa kutoka nchi za kusini mwa Ghuba ya Uajemi. Ripoti zinaonyesha kuwa Saudi Arabia imejitolea kuwekeza dola trilioni moja nchini Marekani, nayo UAE imewasilisha mpango wa kuwekeza nchini humo dola trilioni 1.4 katika kipindi cha miaka 10. Qatar pia imeahidi kuwekeza dola bilioni 300 nchini Marekani. Mikataba hii inajumuisha sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na teknolojia, nishati, miundombinu na ulinzi.
Mikataba hii, haswa katika nyanja za kijeshi, teknolojia na miundombinu, inachukuliwa kuwa muhimu kwa ajili ya kubuni nafasi za ajira na kuimarisha uchumi wa Marekani. Trump anataka kudhihirisha mikataba hii kama ishara ya mafanikio ya sera zake za kibiashara.

Katika hatua yake ya kwanza akiwa Saudi Arabia, Trump alitia saini mikataba mikubwa na ya faida nono kwa Marekani akiwa na Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman. Viongozi wawili hao wakuu wa Marekani na Saudia walihudhuria Mkutano wa Uwekezaji wa nchi hizo siku ya Jumanne, ambao uliambatana na tangazo la kusainiwa mikataba 145 yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 300.
Inatarajiwa pia kwamba Trump atafunga mikataba mingi na mikubwa wakati wa safari yake katika nchi za UAE na Qatar, ambayo bila shaka itayafaidi makampuni ya Marekani kwa mamia ya mabilioni ya dola. Kwa kuzingatia hali hiyo, wamiliki wengi wa makampuni ya Marekani, hasa Elon Musk, bilionea maarufu na Mkurugenzi Mtendaji wa Tesla na SpaceX, wanazikodolea macho ya tamaa fursa ambazo zimeandaliwa kwa ajili yao nchini Saudi Arabia na nchi nyingine za Ghuba ya Uajemi. Kuandamana wasimamizi wa makampuni hayo na Trump katika safari yake ya Ghuba ya Uajemi kunaweza kutathminiwa katika mtazamo huu.
Suala muhimu ambalo linajadiliwa zaidi sasa kuliko huko nyuma kuhusiana na safari ya Trump katika nchi za eneo la kusini mwa Ghuba ya Uajemi ni utegemezi wa kiusalama wa nchi za Kiarabu kwa Marekani. Kwa hakika, licha ya utajiri wao mkubwa, nchi hizi zinatafuta dhamana ya usalama kutoka kwa Marekani. Zinategemea uungaji mkono wa kijeshi na kisiasa wa Marekani kutokana na changamoto za kiusalama za ndani na nje, ikiwemo mivutano ya kikanda na ukosefu wa utulivu wa ndani. Utegemezi huu, wengine wanaamini, umebadilisha uwiano wa nguvu kwa maslahi ya Marekani ambapo nchi hizo zinalazimika kukubali mikataba mikubwa ya kiuchumi pamoja na ununuzi mkubwa wa silaha kutoka Marekani kwa ajili ya kulinda usalama wao.
Kuhusiana na suala hilo, Saudi Arabia ilitia saini mkataba mkubwa zaidi wa mauzo ya silaha katika historia na Marekani, wenye thamani ya dola bilioni 142 ukijumuisha silaha mbalimbali yakiwemo makombora, ulinzi wa anga na mifumo ya kuzuia makombora, magari na ndege za kivita na vifaa vingine vya kijeshi. Mkataba huo, ambao Ikulu ya Marekani iliuita "uuzaji mkubwa zaidi wa silaha za ulinzi katika historia," umetoa fursa ya kipekee na yenye faida kubwa kwa makampuni ya silaha ya Marekani.
Inaonekana kuwa safari ya Trump imeleta manufaa makubwa ya upande mmoja kwa Marekani, na kilichobakia sasa kwa nchi za Kiarabu ni kuwa watumiaji tegemezi tu wa bidhaa za kiuchumi, kisiasa, kijeshi, kisayansi na kiteknolojia za Marekani. Wakati huo huo, safari ya Trump inalenga zaidi kuinufaisha Marekani kiuchumi, kisiasa na kijiografia kuliko kuzisaidia nchi za Kiarabu kutatua masuala yao sugu ya kikanda kama vile mzozo wa muda mrefu wa Wapalestina au mivutano ya kikanda. Aidha, juhudi za kupunguza ushawishi wa China katika eneo hili na kudhibiti soko la nishati (mafuta na gesi) ni malengo mengine yaliyotangazwa ya safari hii, ambayo yatailetea Marekani manufaa chungu tele ya kiuchumi, kisiasa na kimkakati.