Kumalizika operesheni ya kijeshi Tripoli; Libya yaingia tena kwenye mgogoro
Wizara ya Ulinzi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imetangaza kumalizika kwa mafanikio operesheni ya kijeshi huko Tripoli mji mkuu wa nchi hiyo.
Moto wa vita huko Libya uliibuka tena siku ya Jumatatu baada ya kuuawa Abdul Ghani Al-Kakli, Mkuu wa Shirika la Kuunga Mkono Utulivu magharibi mwa Libya. Al-Kalkali alikuwa amekwenda katika makao makuu ya Kikosi cha 444 cha jeshi kwa ajili ya kujadili njia za kudhibiti mvutano unaoongezeka kati ya pande hasimu katika mji huo, lakini mzozo kati ya pande hizo ukaongezeka haraka na kuwa mapigano ya silaha, ambayo hatimaye yalisababisha kifo chake na kupelekea kujeruhiwa watu kadhaa.
Wakati huo huo na sambamba na tukio hilo, eneo la Abu Salim, ambako kuna makao makuu ya Shirika la Kuunga Mkono Utulivu, liligeuka kuwa eneo la mapigano makali kati ya makundi yenye silaha, kadiri kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Serikali ya Umoja wa Kiataifa ya Libya, ambayo inaungwa mkono na Umoja wa Mataifa, iliwataka wananchi kutotoka nje bila dharura ili kulinda usalama wao. Idadi ya vifo katika mzozo huo bado haijajulikana, lakini serikali imetangaza kumalizika kwa operesheni ya kijeshi huko Tripoli na kusema hali imedhibitiwa.
Kurejea kwa mzozo huo licha ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutangaza kuwa inayadhibiti maeneo yenye migogoro, kwa mara nyingine tena kumewafanya watu wazingatie hali ya usalama na mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo ambao haujatatuliwa, nchi ambayo haijawahi kuonja utulivu wa kudumu tangu kupinduliwa kwa utawala wa Muammar Gaddafi mwaka 2011.
Hali nchini Libya si shwari kabisa. Kwa muda mrefu, makundi tofauti ya kijeshi na kisiasa katika maeneo tofauti ya nchi, yanayotafuta mamlaka na ushawishi, hayajaruhusu uchaguzi wa amani na kidemokrasia kufanyika nchini. Kwa hakika, Libya imegawanyika katika sehemu tatu: Libya ya Magharibi, ambayo iko chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Libya ya Mashariki, ambayo iko chini ya udhibiti wa vikosi vya Khalifa Haftar na maeneo ya kusini ambayo hayana utulivu na ni makazi ya makundi ya ukufurishaji na yenye silaha.

Katika mazingira hayo, nchi za eneo na baadhi ya nchi za Magharibi pia zimezuia makubaliano yoyote kufanyika na vilevile mazingira salama ya kufanyika uchaguzi wa rais, kwa kuyaunga mkono makundi ya kisiasa yenye makao yao katika maeneo tofauti ya Libya. Kwa hakika hali ya Libya katika miaka ya hivi karibuni imezifanya nchi nyingi kunufaika moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja na rasilimali, utajiri na maeneo ya kijiografia ya Libya, na hivyo kufunga kikamilifu njia zote za kuleta umoja nchini humo kwa ajili ya kuandaliwa mazingira ya kubuniwa serikali itakayochaguliwa kidemokrasia na wananchi.
Hanna Titi, mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Libya, amewataka viongozi wa Libya pamoja na pande za kigeni kutekeleza wajibu wao na kuruhusu wananchi kuamua viongozi wao kupitia masanduku ya kupigia kura. Akieleza kuwa baadhi ya makundi yenye silaha nchini Libya yanaona manufaa yao yakidhaminiwa kupitia kutofanyika uchaguzi, amesema: "Libya ina rasilimali nyingi za asili na kifedha ambazo zinawawezesha watu wa nchi hii kuishi maisha ya heshima."
Hali hii inakuja wakati miundombinu ya kiuchumi na kijamii ya Libya imeporomoka kabisa. Kukosekana utulivu, kuongezeka machafuko, uvunjifu wa sheria na uwepo wa makundi ya kigaidi kumepelekea hali ya maisha kuwa ngumu kwa watu wa Libya. Kuhusiana na hili, Baraza Kuu la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya hivi karibuni lilisisitiza katika taarifa kwamba, kuendelea migogoro hiyo nchini kumeongeza mateso kwa wananchi, kuharibu miundombinu na uchumi na kuzidisha mgawanyiko unaozuia kuundwa serikali ya kidemokrasia nchini.
Mzozo uliozuka upya nchini Libya na kuuawa kwa Abdul Ghani Al-Kakli, mkuu wa Shirika la Kuunga Mkono Utulivu magharibi mwa Libya, kwa mara nyingine tena kunakumbushia umuhimu wa kuharakishwa mchakato wa kuziunganisha taasisi za serikali ya Libya na kukamilishwa mwenendo wa kukabidhi madaraka kupitia uchaguzi wa kidemokrasia haraka iwezekanavyo. Bila shaka jambo hilo linahitajia kufikiwa makubaliano ya kina kati ya makundi yenye ushawishi mkubwa wa kisiasa na kijeshi nchini. Makubaliano hayo licha ya kuzingatia maslahi ya kitaifa, yanapasa kufanyika chini ya usimamizi na dhamana ya kimataifa ili kuzuia kutokea tena kwa migogoro ya umwagaji damu. Ucheleweshaji wowote katika mchakato huu bila shaka utawanufaisha tu wahusika wa kigeni na makundi ya wabeba silaha ambayo yananufaika zaidi na ombwe la mamlaka yenye nguvu na miundo dhaifu ya kisheria nchini.