Ulaghai wa watawala wa Magharibi; Gaddafi alivyodanganywa na Sarkozy
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130414-ulaghai_wa_watawala_wa_magharibi_gaddafi_alivyodanganywa_na_sarkozy
Moja ya kesi mashuhuri za ulaghai wa watawala wa nchi za Magharibi ni udanganyifu uliofanywa na Nicolas Sarkozy, rais wa zamani wa Ufaransa dhidi ya Muammar Gaddafi, dikteta wa zamani wa Libya.
(last modified 2025-09-05T02:18:59+00:00 )
Sep 05, 2025 02:18 UTC
  • Ulaghai wa watawala wa Magharibi; Gaddafi alivyodanganywa na Sarkozy

Moja ya kesi mashuhuri za ulaghai wa watawala wa nchi za Magharibi ni udanganyifu uliofanywa na Nicolas Sarkozy, rais wa zamani wa Ufaransa dhidi ya Muammar Gaddafi, dikteta wa zamani wa Libya.

Nicolas Sarkozy, alifikishwa mahakamani kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu, akituhumiwa kupokea mamilioni ya fedha kutoka kwa Muammar Gaddafi, dikteta wa zamani wa Libya, ili kugharamia kampeni zake za uchaguzi mwaka 2007. Kesi ya kihistoria ya rais huyo wa zamani wa mrengo wa kulia wa Ufaransa, pamoja na watuhumiwa wengine 12, wakiwemo mawaziri watatu wa zamani wa baraza lake la mawaziri, kwa tuhuma za kupokea pesa kutoka kwa dikteta wa kigeni inachukuliwa kuwa kashfa kubwa zaidi ya kifedha na kisiasa katika historia ya kisasa ya Ufaransa.

Kwa mujibu wa tuhuma zilizotolewa katika kesi ya Sarkozy, watu kadhaa wa karibu na kiongozi huyo wa zamani wa Ufaransa walikutana na maafisa kadhaa wa utawala wa Gaddafi nchini Libya mwaka 2005, wakati Sarkozy alipokuwa bado ni waziri wa mambo ya ndani. Baada ya kushinda uchaguzi wa urais mwaka 2007, alimwalika Gaddafi kwenda Paris na kuweka hema kwa ajili ya dikteta huyo katika moja ya mabustani yaliyo karibu na Ikulu ya Elysee.

Sarkozy alikuwa kiongozi wa kwanza wa Magharibi kumkaribisha Gaddafi baada ya kukatwa uhusiano na kiongozi huyo wa zamani wa Libya katika miaka ya 1980 kutokana na tuhuma za kuunga mkono ugaidi. Hata hivyo, Sarkozy baadaye mwaka 2011, aliiweka Ufaransa katika mstari wa mbele wa mashambulizi ya anga ya NATO dhidi ya vikosi vya Gaddafi, ambayo hatimaye yalipelekea kung'olewa madarakani kwa utawala wa dikteta huyo wa Libya. Gaddafi kisha alikamatwa na kuuawa kinyama katika mapambano ya wananchi yaliyofanyika nchini Libya mwezi Oktoba 2011.

Ulaghai wa nchi za Magharibi

Ushahidi wa kesi ya rushwa ya Sarkozy unaonyesha kuwa mamilioni ya fedha yalihamishwa kinyume cha sheria kutoka kwa utawala wa Muammar Gaddafi hadi kwenye kampeni za urais za Sarkozy mwaka 2007. Mwanasiasa huyo wa kihafidhina, ambaye alikuwa rais wa Ufaransa kuanzia 2007 hadi 2012, amekuwa akikanusha shutuma hizo mara kwa mara.

Kulingana na uchunguzi wa miaka 10, mahakama ilisikiliza madai kwamba masanduku ya pesa yalitumwa na Gaddafi kwenye majengo ya wizara huko Paris. Mwaka 2007, Sarkozy alipokea kwa siri euro milioni hamsini kutoka kwa Gaddafi kwa ajili ya kugharamia kampeni zake za uchaguzi. Kwa mara ya kwanza, Saif al-Islam, mtoto wa Muammar Gaddafi, alifichua suala hili mwaka 2011 akimtuhumu Sarkozy kwa kupokea kiasi hiki kikubwa cha fedha.

Kashfa ya rushwa kubwa ya Gaddafi kwa Sarkozy, ambaye alikula hongo hiyo kwa ahadi za kurekebisha uhusiano wa Libya na nchi za Magharibi, pamoja na kuondolewa tuhuma dhidi ya viongozi wa Libya katika kesi mbalimbali na muhimu zaidi, kudhaminiwa uungaji mkono wa Ufaransa kwa utawala wa Gaddafi, inathibitisha wazi, hasa kufuatia harakati za watu wa Libya za mwaka 2011 na hatimaye kushambuliwa Libya na nchi za NATO, ikiwemo Ufaransa, kwamba wanasiasa wa nchi za Magharibi ambao si waaminifu wala kuwa na dhamira ya kimaadili, hawazipi umuhimu wowote nchi nyingine za dunia hasa  zile zinazochukuliwa kuwa za ulimwengu wa tatu kama Libya. Hivyo walimdanganya kirahisi Muammar Gaddafi, na hatimaye, kumtupilia mbali, kama ganda la chungwa linatupwa pembeni baada ya kukamuliwa juisi iliyomo.