Iran: Hakuna haja ya kuendelea na mazungumzo iwapo Marekani....
(last modified Wed, 14 May 2025 11:30:54 GMT )
May 14, 2025 11:30 UTC
  • Iran: Hakuna haja ya kuendelea na mazungumzo iwapo Marekani....

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi amesisitiza kuwa haki ya Jamhuri ya Kiislamu ya kurutubisha madini ya urani ni "mstari mwekundu" wa taifa hili, akisisitiza kuwa, kufikiwa makubaliano na Marekani kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa nchi hii kunategemea kufuata kanuni hizo.

Ebrahim Rezaei, Msemaji wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Bunge la Iran, ameashiria kuwa, Gharibabadi amesema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari jana Jumanne kuhusu duru ya nne ya mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja ya Tehran na Washington nchini Oman mwishoni mwa juma.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alinukuliwa na Rezaei akisema kuwa, "kanuni na mambo ya jumla" yalijadiliwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika duru ya nne ya mazungumzo, na Jamhuri ya Kiislamu ilisisitiza tena mistari yake myekundu katika mazungumzo hayo.

"Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika Sheria na Masuala ya Kimataifa amesema kwamba, urutubishaji wa urani ni mstari mwekundu kwa Jamhuri ya Kiislamu, na kwamba hakuna mazungumzo yaliyofanyika kuhusu masuala ya kikanda au nguvu za ulinzi na makombora (ya Iran)," Rezaei amesema.

Gharibabadi amenukuliwa akisema, Iran pia imekosoa "misimamo inayokinzana ya Wamarekani na vikwazo vyao vya hivi majuzi", na akasisitiza kwamba "ili kufikia makubaliano, ni sharti kuzingatia misimamo myekundu ya Iran; kwa hivyo, ikiwa Wamarekani hawataki turutubishe urani, hatuoni haja ya kuendelea na mazungumzo." 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria umuhimu na ulazima wa urutubishaji wa urani wa ndani, akisema, "Urutubishaji wa urani unafungamana na fahari ya kitaifa ya Wairani na tumelipa sana umuhimu upatikanaji wa teknolojia hii, kwa hivyo ni mstari mwekundu kwa nchi na hatutarudi nyuma," Rezaei ameeleza akimnukuu Gharibabadi.