Pezeshkian: Vita vingeenea Mgharibi mwa Asia kama uchokozi wa Wazayuni usingejibiwa
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kuwa vita vya pande zote vingeshuhudiwa katika eneo zima la Magharibi mwa Asia iwapo hujuma ya uchokozi wa Israel ingesalia bila ya jibu.
Rais Pezeshkian alieleza haya jana katika Kongamano la Nne la Kiuchumi la Eurasia lililofanyika kwa njia ya video huko Minsk, nchini Belarusia.
Amesema, vikosi vya ulinzi vya Iran vilitoa jibu halali kwa hatua ya Israel ya kushambulia ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu, kwa mujibu wa kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa.
Israel ilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya ardhi ya Iran huku mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington yakiendelea kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani.
Rais wa Iran ameongeza kuwa mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na utawala wa Israel dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran vinavyoendesha shughuli zake kwa malengo ya kiraia na amani, ambavyo vimekuwa chini ya usimamizi kamili wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ni ukiukaji wa wazi wa sheria na kanuni zote za kimataifa.
Pezeshkian ameitaka jamii ya kimataifa hasa Baraza la Usalama la UN na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) kuwajibika ipasavyo mkabala wa pande vamizi na waanzishaji vita.