Je, vita vya Israel dhidi ya Iran vilikuwa na sifa zipi maalumu?
Vita vya siku 12 vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vina sifa maalumu zinazotofautiana na vita vingine vya kieneo.
Vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran vimejiri katika hali ambayo hakuna uhusiano wowote wa kidiplomasia uliopo kati ya Tehran na Tel Aviv. Uadui wa Iran na Israel hauna mfano wake kati ya mahasimu wawili katika mfumo wa dunia. Suala jingine ni kwamba; hadi sasa vita na mizozo ya kieneo imekuwa ikitokea baina ya nchi zilizo na mpaka wa pamoja wa kijiografia, kama vile vita vya Iran na Iraq, vita vya utawala wa Kizayuni na Lebanon na Palestina, na vita kati ya Syria na Misri na utawala wa Kizayuni. Utawala huo unaokalia Quds Tukufu kwa mabavu umeanzisha vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, licha ya kutokuwa na mpaka wa pamoja nayo, ambapo una umbali wa kijiografia wa takriban kilomita 1,500.
Umbali huu wa kijiografia ulizuia mapigano yoyote ya nchi kavu kati ya pande hizi mbili wakati wa siku 12 za vita. Hii inaweza kuchukuliwa kuwa moja ya fursa ulizokuwa nazo utawala wa Kizayuni katika vita hivi. Bila shaka, kama kungekuwa na uwezekano wa kutokea vita vya nchi kavu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ingeweza kutoa pigo kubwa zaidi kwa Tel Aviv.
Sifa nyingine ni kwamba teknolojia bora za kijeshi zilitumika katika vita hivi. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitumia ndege zisizo na rubani na teknolojia ya kuongoza makombora ya masafa marefu, kutoka ardhini hadi angani, huku utawala wa Kizayuni ukitumia ndege za kivita, ndege nyuki, makombora na ndege zisizo na rubani, yaani droni. Tofauti kubwa ni kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitumia silaha na zana zilizotengenezwa na wanasayansi wake wa ndani ya nchi, ambapo aghalabu ya zana zilizotumiwa na utawala wa Kizayuni ziliagizwa kutoka nchi za Magharibi hususan Marekani.
Sifa nyingine makhsusi ya vita hivyo ni kwamba utawala wa Kizayuni uliingia vitani kwa niaba ya nchi za Magharibi na ukapata uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani, baadhi ya nchi za Ulaya, na hata shirika la NATO, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipigana kwa ajili ya kulinda mipaka na usalama wake na wala haikuwa nguvu ya niaba kwa maslahi ya wahusika wengine. Kwa hakika, Vita vya Siku 12 vimeonyesha kuwa utawala wa Kizayuni unaweza tu kupambana na wachezaji wadogo katika eneo la Asia Magharibi bila kuhitajia msaada wa Marekani. Utawala huu umeonyesha kuwa hauna ubavu wa kusimama dhidi ya nchi yenye nguvu kubwa kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hata kwa uungaji mkono wa Marekani na nchi Ulaya.
Sifa nyingine ya vita hivi ni kwamba vilitishia uwepo wa pande zote mbili. Utawala wa kibaguzi wa Israel uliingia vitani kwa lengo la kubadilisha mfumo wa kisiasa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini haukuweza kufanya lolote kwa sababu haukutarajia kwamba vita hivyo vingepelekea kuimarika zaidi mshikamano na umoja wa kitaifa nchini Iran. Vita hivi pia vilikuwa tishio kwa uwepo wa utawala wa Kizayuni.
Jambo jingine muhimu ni kwamba mwisho wa vita kati ya Tel Aviv na Tehran haukutangazwa, bali vita vimesitishwa tu. Kwa hiyo, vita vinaweza kupamba moto tena kati ya pande hizi wakati wowote. Cheche moja tu inatosha kuwasha tena vita. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imethibitisha kuwa haikuanzisha vita hivyo, ambapo vita vya siku 12 vimethibitisha kwamba Iran haitajizuia tena au kuwa na subira ya kimkakati mbele ya ukiukwaji mdogo wa mamlaka yake, bali itajibu uchokozi wa aina yoyote kwa nguvu zake zote na bila kusita.