Araghchi: Msamiati wa ‘Kusalimu Amri’ haumo kwenye fasihi ya watu wa Iran
(last modified Sat, 28 Jun 2025 06:30:36 GMT )
Jun 28, 2025 06:30 UTC
  • Araghchi: Msamiati wa ‘Kusalimu Amri’ haumo kwenye fasihi ya watu wa Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Abbas Araghchi amesema, kama alivyobainisha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, hakuna msamiati wa kusalimu amri katika fasihi ya kisiasa na fasihi ya wananchi wa Iran na kwamba wananchi hao wamethibitisha na kulionyesha vizuri hilo katika kipindi cha siku 12.

Sayyid Abbas Araghchi ameeleza: “wavamizi walidhamiria kuwasambaratisha wananchi wa Iran, lakini katika siku hizi 12 tumeshuhudia Muqawama wa pamoja wa wananchi wa Iran, ambao wameuonyesha ulimwengu kwamba Iran na Wairan hawawezi kushindwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria sera ya mashinikizo ya juu kabisa iliyotekelezwa na serikali ya Marekani dhidi ya Iran kwa miaka yote hii ili Iran isiweze kunufaika na haki yake; na akaongezea kwa kusema: “katika mazungumzo pia walijaribu kuturubuni ili tuachane na haki zetu, lakini walipoona hawajapata walilokusudia waliamua kutumia wenzo wa kijeshi dhidi ya taifa la Iran kwa kuuruhusu utawala wa Kizayuni uishambulie kijeshi Iran”.

Huku akisisitiza kuwa kwa kitendo chake hicho Marekani imeisaliti diplomasia, Araghchi amesema: “katika kipindi kile, sisi tulichagua njia ya mazungumzo ili kutimiza dhima kwa ulimwengu na kuonyesha kuwa ni wakweli kwa kutoondoka kwenye meza ya mazungumzo, lakini wao wameisaliti diplomasia”.

Mkuu wa vyombo vya diplomasia vya Iran amezishukuru pia nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai, BRICS na nyinginezo kwa kuchukua msimamo wa kulaani mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran na akasema, tulichojitahidi kufanya ni kuonyesha haki ya wananchi wa Iran.

Araghchi amemalizia kwa kusema: siku hizi 12 inapasa zitambulike kama nembo ya Muqawama ya taifa lililosimama kukabiliana na madola  yaliyosimama nyuma ya utawala wa Kizayuni huku yakitoa msaada na kuunga mkono mashambulizi hayo…/