Baqaei: Matakwa ya Wairani ya haki na uadilifu hayatafifia
(last modified Sun, 29 Jun 2025 08:05:15 GMT )
Jun 29, 2025 08:05 UTC
  • Baqaei: Matakwa ya Wairani ya haki na uadilifu hayatafifia

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, matakwa ya Wairani ya ukweli na uadilifu hayatafifia, kwa sababu jinai za kivita na jinai dhidi ya ubinadamu hazitapitwa na wakati.

Ismail Baqaei amesema hayo kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka wa 38 wa shambulio la kemikali la utawala Saddam wa Iraqa dhidi ya mji wa Sardasht wa Iran.

Ismail Baqaei, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, ameandika kwenye akaunti yake ya X: Leo ni kumbukumbu ya miaka 38 ya shambulio la silaha za kemikali la Saddam huko Sardasht kaskazini magharibi mwa Iran. Hii haikuwa mara ya kwanza kwa dikteta huyo wa Iraq kutumia silaha za kemikali katika vita vyake vya uvamizi dhidi ya Iran.

Baadhi ya wahanga wa shambulio la silaha za kemikali la utawala wa Baath dhidi ya mji wa Sardasht wa Iran

 

Aliendelea kusema: Katika kipindi cha miaka minane ya vita vya kulazimishwa, jeshi la Saddam liliwashambulia mara kwa mara wanajeshi na raia wa Iran kwa kutumia silaha za kemikali bila kuhojiwa na kuadhibiwa na jamii ya kimataifa. Miaka 38 baada ya tukio hilo, Wairani bado wanadai ufafanuzi wa ukweli na utekelezwaji wa haki  na uadilifu kwa wale walioupa utawala wa Saddam silaha za kemikali.

Utawala wa Baath wa Iraq Juni 28 mwaka 1987 ulitumia mabomu ya kemikali kushambulia maeneo manne ya kaunti ya Sardasht katika mkoa wa Azerbaijan Magharibi, unaopatikana kaskazini magharibi mwa nchi. Raia 119 wa eneo hulo waliuawa shahidi na wengine zaidi ya 8,000 walidhurika kwa gesi ya sumu na kupata maradhi ya aina mbalimbali.