China kwa Marekani: Tutajidhaminia nishati kwa kuzingatia maslahi ya kitaifa
Akijibu matamshi ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani kwamba Beijing inaweza kununua mafuta kutoka Tehran, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesisitiza kuwa nchi yake inajidhaminia nishati kwa kuzingatia maslahi yake ya kitaifa.
Guo Jiakun amesema: "China itachukua hatua zinazofaa ili kuhakikisha kuna usalama wa nishati kwa kuzingatia maslahi yake ya kitaifa."
Matamshi haya yanakuja wakati Washington inaendelea kusisitiza juu ya vikwazo vya mafuta dhidi ya Iran na kusema ushirikiano wowote wa kiuchumi na Tehran unapasa kutilia maanani vikwazo hivyo.
China na Iran zimekuwa na uhusiano mkubwa wa mafuta kwa miongo kadhaa, uhusiano ambao umekuwa ukiimarika zaidi katika miaka ya hivi karibuni, licha ya vikwazo vya Marekani.
Tangu 2018, Iran imekuwa moja ya wauzaji wakuu wa mafuta kwa China, ambapo makampuni ya nchi hiyo yameshiriki vilivyo katika kustawisha visima vya mafuta vya Iran. Kwa mujibu wa ripoti mpya mwaka huu, uuzaji wa mafuta ya Iran kwa China umefikia rekodi ya zaidi ya mapipa milioni 1.46 kwa siku.