Maandamano ya waungaji mkono wa Iran yautikisa mji wa Vienna
Maelfu ya wanaharakati wanaopinga vita na watu wa matabaka tofauti nchini Austria walifanya maandamano Jumamosi ya jana, Juni 28, katika mitaa ya kati ya Vienna kuelezea mshikamano wao na Iran mkabala wa mashambulizi ya Marekani na Israel.
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba picha za wahanga wa mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya Iran, walitoa mwito kukomeshwa mara moja vitendo vya kichokozi vya utawala wa Kizayuni.
Kadhalika, kundi la wanaharakati wa Kiyahudi wenye chuki dhidi ya Uzayuni walishiriki katika maandamano hayo na kusisitiza kuwa, jinai za Israel hazina uhusiano wowote na dini ya Kiyahudi.
Washiriki wa maandamano hayo ya kuunga mkono Iran na kulaani uchokozi wa Israel wameitaka jamii ya kimataifa kutonyamaza kukabiliana na uchokozi huu.
Wiki iliyopita, maandamano kama hayo yalifanyika Vienna na miji mingine kadhaa ya Ulaya, ambapo waandamanaji walikosoa undumakuwili wa madola ya Magharibi.
Ijumaa ya tarehe 13 Juni, utawala haramu wa Israel ulianzisha uchokozi kwa kufanya mashambulio dhidi ya ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu na kupelekea kuuawa maafisa kadhaa wa kijeshi wa ngazi za juu na raia wa kawaida.
Baada ya uchokozi huo, Iran ilianzisha Operesheni ya Ahadi ya Kweli-3 na kutoa majibu makali dhidi ya utawala haramu wa Israel kwa kuvurumisha makombora yaiyosababisha mauaji na uharibifu mkubwa dhidi ya miji ya Tel Aviv na Haifa na kuulazimisha utawala huo ukubali usitishaji vita.