Russia: Teknolojia ya nyuklia ya Iran haiwezi kuharibiwa kwa mabomu
Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia akizungumzia mashambulizi ya karibuni ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran vinavyoendesha shughuli zake kwa malengo ya amani amesisitiza kuwa, ujuzi, uzoefu, teknolojia na utashi wa kisiasa wa Iran hauwezi kuharibiwa kwa mabomu.
Ryabkov ameeleza kuwa licha ya ukweli kwamba kuna uharibifu ambao umefanyika kwenye mitambo ya nyuklia ya Iran lakini wakati huo huo mashambulizi ya utawala wa Kizayuni na Marekani kwenye vituo hivyo hayawezi kuharibifu mpango mzima wa nyuklia wa Iran.
Sergei Ryabkov amebainisha kwambva licha ya kuwa mashambulizi haya yamekuwa makali na makubwa lakini ni wazi kuwa ujuzi wa nyuklia wa Iran hauwezi kufutwa kwa mashambulio kama hayo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia aidha ameashiria kwamba wanasiasa wa Israel na Marekani wanajaribu kujiridhisha kwamba madai yao yamekuwa ya kweli na kusema: "Kuna nchi nyingine kadhaa zisizo wanachama wa Mkataba wa Kuzuia Usambazajai wa Silaha za nyuklia NPT ambazo zina vituo vya kisasa zaidi vya nishati ya nyuklia kuliko Iran, lakini haziandamwi wala kuibua wasiwasi wa kimataifa."
Sergei Ryabkov ameutaka utawala wa Kizayuni ujiunge na mkataba wa NPT na kuongeza: "Kwa hakika Iran ambayo haina silaha za nyuklia imeshambuliwa mara mbili na pande zinazomiliki silaha hizo."