Mkutano wa 31 wa Nyuklia wa Iran wafunguliwa mjini Mashhad
Mkutano wa 31 wa Nyuklia wa Iran, ulioandaliwa na Jumuiya ya Nyuklia ya Iran na kuungwa mkono na Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI), umefunguliwa katika mji wa Mashhad, uliopo kaskazini-mashariki mwa Iran.
Miongoni mwa mada kuu za tukio hili la kisayansi ni “Matumizi ya Mionzi na Teknolojia Mpya za Mionzi”, “Fizikia na Teknolojia ya Muungano wa Nyuklia na Plasma”, “Majenereta ya Nyuklia na Teknolojia za Quantum”, “Mzunguko wa Mafuta ya Nyuklia na Vifaa”, na “Utawala wa Nyuklia na Maendeleo Endelevu”.
Mkutano huu unatarajiwa utakamalizika Mei 15 na utatoa fursa ya kubadilishana mawazo, kuonyesha mafanikio mapya, na kukuza ushirikiano wa kitaifa katika sekta ya sayansi na teknolojia ya nyuklia.
Mada kuu zitakazozungumziwa katika siku ya kwanza ya mkutano ni pamoja na: "Majenereta ya Utafiti Duniani na Matumizi Yao”, “Utangulizi Kuhusu Mfumo wa Picha za Neutron katika Kituo cha Nyuklia cha Utafiti cha Tehran”, “Uzalishaji wa Radioisotopi katika Kituo cha Nyuklia cha Utafiti ”, na “Utangulizi Kuhusu Kituo cha Nyuklia cha Utafiti cha Isfahan.”
Akizungumza na baraza la mawaziri Jumapili, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian alisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu, chini ya hali yoyote, haitakubaliana na kupunguzia uwezo wake wa nyuklia katika mazungumzo na Marekani.
Amesema ushirikiano wa Iran katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani unaonyesha kuwa Tehran inajitolea kwa amani.
Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa Iran haitakubali kuachana na vituo vyake vya nyuklia na ameongeza kwamba teknolojia ya nyuklia na maendeleo yaliyofanywa na wanasayansi wa Iran katika sekta ya nyuklia ya amani yana matumizi katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kilimo, uhifadhi wa mazingira, viwanda, na tiba.
Kwa hiyo, amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kwa uthabiti na shughuli zake za nyuklia za amani.
Rais Pezeshkian amefafanua kuwa Iran haijawahi kutaka, na kamwe haitotaka silaha za nyuklia, akisema kuwa inapingana na silaha hizo.