Ghana yajibu mapigo kwa Israel, yawatimua wazayuni watatu waliowasili nchini humo
Serikali ya Ghana imewatimua kwa kuwarejesha walikotoka Waisraeli watatu, katika hatua ya kujibu mapigo na kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa kizayuni wa Israel baada ya hapo awali kulalamikia kunyanywaswa raia wake katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion, mjini Tel Aviv.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ghana imesema: “Serikali ya Ghana imewajibika kuchukua hatua hiyo baada ya raia wake kunyanyaswa na Israel…tutaendelea kulinda utu na heshima yetu”.
Taarifa hiyo iliyotolewa jana Jumatano imebainisha kuwa, raia hao watatu wa Israel waliwasili nchini humo mapema jana hiyohiyo.
Serikali ya Ghana imesisitiza kuwa, raia wake wanastahili kupewa heshima kama nchi zingine zinavyotarajia pale raia wao wanapoingia Ghana.
Mapema Jumatano, serikali ya Ghana ililaani kitendo cha kunyanyaswa raia wake kwenye uwanja wa ndege wa Ben Gurion huko Tel Aviv, hali iliyopelekea baadhi ya abiria ndani ya uwanja huo kuwekwa rumande.
Kwa mujibu wa serikali ya Accra, raia wake saba, wakiwemo wajumbe kutoka bunge la nchi hiyo, waliwekwa vizuizini bila sababu za msingi, na baadaye kuachiwa, huku wengine watatu wakirejeshwa nchini kwao..../