Ulimwengu wa Michezo
Karibuni mashabiki na wapenzi wa michezo popote pale mlipo katika kipindi chenu hiki cha Ulimwengu wa Michezo kutoka Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran. Leo kapu letu la habari za michezo limesheheni habari kemkem kama ilivyo ada na desturi yake. Mimi ni Ahmed Rashid, karibuni.
Wiki hii tunaanza na habari ya kiroja cha viroja katika ulimwengu wa michezo. Tunaanza na habari iliyopata umaarufu wa jina la 'Joki ya Karne.' Hiyo ni habari gani iliyoenea kama moyo wa nyika kavu? Ni kioja cha karne cha tunzo ya kwanza ya Amani ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA. Nyota njema huonekana alfajiri, lakini hii tunzo ya amani ya kwanza kabisa ya FIFA imeonesha si nyota njema na haibashiri jema lolote katika siku zijazo. Imekuwa ni kioja cha vioja tunzo hiyo kupewa muhusika mkubwa wa umwagaji damu duniani, rais wa Marekani Donald Trump kwa jina la mpenda amani. Hayo sisemi mimi, bali watumiaji wa mitandao ya kijamii wanasema kwamba hatua ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ya kumpa Tuzo ya Amani rais wa Marekani Donald Trump ndito habari ya kipuuzi zaidi ambayo wamewahi kusikia katika maisha yao yote. Wanaharakati wa kimataifa wameudhihaki uamuzi wa FIFA wa kumpa Trump Tunzo ya Amani tena ya kwanza kabisa kuwahi kutolewa na shirikisho hilo la soka duniani. Vibonzo vimeenea kwenye mitandao ya kijamii kukebehi hatua hiyo ya FIFA.
Wakizungumzia jinsi rais huyo wa Marekani alivyotuma silaha zinazotumiwa na Israel katika mauaji ya kimbari ya Wapaletina wa Ukanda wa Ghaza, jinsi alivyoshindwa kuchukua hatua za kivitendo za kuzuia vita vya Ghaza kwa wakati mwafaka na mienendo yake mingine ya kivita dhidi ya nchi nyingine kama Venezuela, wadau wa mitandao ya kijamii wameitaja hatua ya FIFA kuwa ni mchezo wa kisiasa unaosambaratisha itibari ya shirika hilo la kimataifa.
Tuzo ya kwanza ya Amani ya FIFA ilitangazwa Disemba 5, 2025 kwa mara ya kwanza, na kupewa wa rais wa Marekani, Donald Trump, wakati wa hafla ya droo ya Kombe la Dunia. Hapa tutanukuu baadhi ya yaliyolalamikiwa na mashabiki wa soka duniani.
Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekitaja kitendo hicho cha FIFA kuwa ni kielelezo cha udhaifu jinsi shirikisho hilo la kimataifa la mpira wa miguu lilivyo tegemezi, wakisisitiza kwamba kumpa Tunzo ya Amani mtu kama Trump kumebandika kovu la fedheha na aibu katika kipaji cha FIFA. Vileve wametoa mwito wa kususiwa mashindano ya Kombe la Dunia yatakayofanyika mwakani katika nchi tatu za Marekani, Mexico na Canada.
Mmoja wa watumiaji wa mitandao ya kijamii amesema: Hatua ya FIFA kumpa Trump Tuzo ya Amani ni kichekesho cha karne.
Mdau mwingine wa mitandao ya kijamii amesema: Baada ya Trump kupewa Tuzo ya amani ya FIFA, huwenda pia Shirikisho la Soka Duniani likatoa tuzo hiyo kwa Wazayuni wa Israel kwa kuwaua kwa kimbari Wapalestina!
Mtumiaji mwingine ameandika: "Dunia hii inaonekana kutawaliwa na watu makatili. Sasa tunzo hazitolewi kwa msingi wa kutenda wema, bali kwa msingi wa maslahi na faida. Haijalishi anayepewa ni muovu kiasi gani, atapewa tunzo tu maadamu ana faida na maslahi kwa watoaji tunzo hiyo. Mwengine amesema: Uamuzi huo wa FIFA umeonekana kama jaribio la kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi na Trump, na wengi wameutambua kuwa ni "kujipendekeza na kujikomba FIFA kwa kiongozi huyo wa Marekani."
Kwa upande wake, mwanaharakati wa haki za binadamu Craig Gerard Mokhiber amesema katika mahojiano na televisheni ya Al Jazeera kwamba: "Baada ya miaka miwili ya kushiriki FIFA katika mauaji ya kimbari ya Palestina, Mkuu wa FIFA Infantino na washirika wake sasa wamebuni tuzo mpya ya amani ili kujiunga na Trump." Ukosoaji huo unarejea nyuma katika uhusiano mkubwa wa Gianni Infantino na Donald Trump, ambao ulianza tangu Marekani ilipofuzu kura ya kuandaa mashindano ya Kombe la Dunia FIFA 2026 na unajumuisha mikutano ya mara kwa mara wa wawili hao na kuungana mkono pande hizo mbili. Gazeti la The Guardian limeandika katika makala ya kejeli kwamba: "Trump ashinda Tuzo ya Amani ya FIFA - je, VAR inaweza kuibatilisha?" Kiujumla yamesema mengi kuhusu kioja cha viroja kilichofanywa na FIFA cha kumpa tunzo ya amani mtu kama Donald Trump na wote kauli yao ni moja, FIFA na hasa Infantino wanajikomba kwa rais huyo wa Marekani.
******
Tunaendelea mbele na kipindi hhiki cha Ulimwengu wa Michezo kwa habari ya mashindano ya Kimataifa ya Taekwondo ya vijana wa chini ya miaka 21 yaliyofanyika jijini Nairobi Kenya. Timu ya wavulana ya Iran imetwaa ubingwa wa mashindano hayo. Naam, Timu ya wavulana ya Iran imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Dunia ya Taekwondo ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 21 ya 2025 yaliyofanyika jijini Nairobi, Kenya. Timu ya wavulana ya Iran imetwaa taji hilo baada ya kushinda medali tatu za dhahabu, moja ya fedha, na mbili za shaba. Mashindano hayo, yalianza Jumatano kwa kushiriki washindani 452 wa taekwondo kutoka nchi 75 duniani na kumalizika Jumamosi kwa mashindano ya mwisho katika kategoria za wanaume za kilo −68 na kilo −78 na kategoria za wanawake za kilo −46 na kilo −62.
Chini ya uongozi wa Majid Aflaki, timu ya wavulana ya Iran iliongoza kwenye msimamo kwa kukomba medali tatu za dhahabu, fedha moja na shaba mbili. Uturuki ilimaliza ya pili kwa kutwaa dhahabu mbili na fedha moja, ikifuatiwa na Kazakhstan kwa medali moja ya dhahabu mbili fedha na shaba moja. Misri, Bulgaria na India zilishika nafasi zilizofuata.
Timu ya wasichana ya Iran yenye washiriki sita, inayofundishwa na Mahrouz Saei, ilimaliza mashindano hayo ya jijini Nairobi kwa dhahabu moja na shaba moja ikishika nafasi ya nne nyuma ya Uturuki, Korea Kusini na Morocco. Mwishoni mwa shindano, Aflaki alihepewa tunzo ya Kocha Bora wa Taekwondo.
******
Habari nyingine fupi kwa leo ni hii inayosema: Njia ya kuelekea Kombe la Dunia la FIFA la 2026 sasa iko wazi kwa Iran baada ya droo ya Ijumaa usiku huko Washington, D.C., iliyoiweka Timu ya Taifa ya Iran maarufu kwa jina la Time Melli katika Kundi G lenye timu za taifa za Ubelgiji, Misri na New Zealand. Hafla hiyo, iliyofanyika katika Kituo cha John F. Kennedy, iliwakutanisha Rais wa FIFA Gianni Infantino, nyota wa zamani wa mpira wa miguu duniani na wajumbe kutoka mataifa yote 48 yaliyofuzu fainali za kombe la dunia.
Habari nyingine muhimu ya Michezo ni kwamba, licha ya kuwa kila linapokuja jina Palestina linawakumbusha walimwengu maafa wanayopitia wanachi madhlumu wa taifa hilo kutoka kwa Wazayuni wa kimataifa ambao hakuna jinai ambayo hawajawahi kuifanya dhidi ya Wapalestina, lakini katika upande mwingine, wananchi wa Palestina nao wamo kwenye fani nyinginezo mbalimbali na wako vizuri. Miongoni mwa habari zenye matumaini ni hii inayosema kwamba, Timu ya Taifa ya Palestine imeingia robo fainali ya Kombe la Kiarabu la FIFA huku Qatar ikitolewa. Mabingwa wa Asia Qatar wametolewa kwenye Kombe la Kiarabu la FIFA 2025 baada ya kuchezea kipigo cha mabao 3-0 mbele ya Tunisia, huku Palestine ikisonga mbele na kuingia robo fainali kwa mara ya kwanza kwa sare ya 0-0 dhidi ya Syria. Majanga ya Qatar yalianza mapema sana tangu kwenye mechi ya ufunguzi ya mashindano hayo kwa kuchezea kipigo cha bao moja kwa nunge katika mechi ya ufunguzi wa Kombe la FIFA la nchi za Kiarabu. Palestina ilipata ushindi huo wa 1-0 dhidi ya wenyeji wa mashindano hayo yaani Qatar katika mchezo wao wa ufunguzi wa Kombe la FIFA la nchi za Kiarabu A, kwa bao la kujifunga la mlinzi wa Qatar Sultan Al Brake katika dakika ya tano ya muda wa nyongeza wa kipindi cha kwanza.
******
Tunaelekea barani Afrika. Miongoni mwa habari muhimu za Michezo wiki hii ni mechi iliyopiga Disemba 7 kati ya Azam na Simba Sports Club, vijana wa Msimbazi. Baada ya mechi hiyo, vyombo vya habari vya Tanzania vimekuja na kichwa cha habari kama hiki: Azam yaifumua Simba. Mechi bora ya Ligi Kuu Bara ilipigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na Azam ilimaliza ubabe wa Simba kwa kuichapa mabao mawili kwa nunge. Huo ulikuwa mchezo muhimu kwa zimu zote mbili kuhakikisha zinajiweka kwenye mazingira mazuri katika Ligi Kuu Bara lakini pamoja na kosakosa za kila mara bado timu zote mbili zilishindwa kutikisa nyvu kwenye dakika 45 z kipindi cha kwanza. Mabao yote mawili ya Azam dhidi ya Simba yalifungwa kwenye kipindi cha pili. Ikumbukwe kuwa timu ya sima hivi sasa iko kwenye mgogoro baada ya kumtimua kocha wake Dimirat Pantev na sasa inasaka kocha mpya wa kukinoa kikosi hicho.
Kwa huko nchini Kenya, nyasi zilipata tabu wakati watani wa jadi, Gormahia na AFC Leopards ziliponyukana. Leopards hawakuwaonea huruma watani wao wa jadi. Waliwachapa mabao 4-1 na kumlazimika kocha wa Gormahia, Charles Akonnor kuwaomba radhi mashabiki wa timu yake kwa kipigo hicho kikali.
*******
Wiki hii pia mambo hayakuendea vizuri timu ya Real Madrid ya Uhispani baada ya kukubali kipigo cha mabao mawili kwa bila mbele ya Celta Vigo. Matokeo hayo yameongeza pengo la pointi nne kati ya Madrid na Barcelona iliyoko kileleni kwenye msimamo wa ligi maarufu kwa jina la La Liga. Hali haikuwaendea vizuri pia Arsenal huko Uingereza baada ya bao la dakika za nyongeza kuwakosesha pointi muhimu za kujikita zaidi kileleni. Arsenal ilifungwa mabao mawili kwa moja na Aston Villa. Arsenal bado inaongozwa msimamo wa ligi ya Premier kwa poingi 28 iliguatiwa na timu za Machester Ciry, Aston Bila na Crysital Palace.
Kuna na hii habari nyingine ambayo ni vyema tuigusie hapa. Uhusiano wa Mohamed Salah mchezaji nguli wa Liverpool raia wa Misri na timu yake hiyo unazidi kuwa mbaya siku baada ya siku baada ya Salah kusema kuwa, "ametupwa chini ya basi" alipokuwa akiingia ndani ya klabu hiyo na kuashiria uwezekano wa kuachana na timu hiyo, baada ya kutazama akiwa kwenye benchi wakati timu yake ilipolazimishwa sara ya mabao 3-3 na Leeds United Jumamosi. Akizungumzia mehi hiyo, Salah, 33, alimkosoa kocha Arne Slot, akiwaambia waandishi wa habari kwamba anahisi amebezwa na huenda akahama Anfield alipopazoea kwa kuwepo hapo kwa muda mrefu.
"Niwe mkweli, kwa hakika nimesikitishwa sana. Nimeifanyia mambo mengi timu yangu hii, kila mtu anaweza kuona hilo katika miaka hiyo na hasa msimu uliopita," Salah aliwaambia waandishi wa habari. "Sijui, inaonekana kama klabu inanitupa chini ya basi. Hivi ndivyo nilivyohisi, ndivyo ninavyohisi."
"Nadhani ni wazi sana kwamba kuna mtu anataka nilaumiwe mimi." Klabu iliniahidi katika msimu wa joto, ahadi nyingi lakini haijanitekelezea kitu chochote hadi sasa.”
Mmisri huyo, ambaye alisaini mkataba wa miaka miwili mwezi Aprili, amekuwa mtu maarufu katika kipindi cha miaka minane akiwa Liverpool ambapo alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu na kufunga mabao 250 katika mashindano yote kwa klabu hiyo.
Hata hivyo, hivi sasa ameshawekwa beni kwenye mechi tatu na amechezeshwa dakika 45 tu. Timu yake ya Liverpool inaboronga hivi sasa, iko ya tisa katika msimamo wa ligi.
Ni hayo kwa wiki hii mashabiki wa michezo wa Idhaa ya Kiswahili, Radio Tehran.