UNIFIL yapinga madai ya Israel kuhusu silaha za Hizbullah
Kamanda wa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL) amesema kuwa ujumbe wa kulinda amani wa kimataifa haujapata ushahidi wowote kuhusu Harakati ya Hizbullah kujenga upya uwezo wake wa kijeshi, akikanusha madai ya Israel yaliyotumika kama kisingizio cha kushambulia kusini mwa Lebanon.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Channel 12 cha Israel Jumatatu, Diodato Abagnara alisema hakukuwa na "ushahidi" kwamba harakati hiyo ya Muqawama ya Lebanon ilikuwa ikijizatiti kwa silaha tena kusini mwa Mto Litani.
Abagnara, ambaye alichukua wadhifa kuongoza UNIFIL mwezi Juni, pia alikosoa mashambulizi ya angani ya Israel dhidi ya Lebanon, ambayo yameua mamia ya watu, akisema kuwa yanakiuka waziwazi makubaliano ya kusitisha mapigano.
Alionya kuwa kosa dogo linaweza kusababisha kushadidi kwa ghasia, akielezea hali ya usalama kuwa “nyeti sana.”
Abagnara aliongeza kusema kuwa uwepo wa wanajeshi wa Israel katika maeneo matano kando ya Line ya Buluu, inayopambanua mpaka kati ya Lebanon na maeneo yaliyokaliwa na Israel, ni dhidi ya azimio la Umoja wa Mataifa nambari 1701.
Azimio hilo, lililosaidia kusitisha vita vya siku 33 vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya Lebanon mwaka 2006, linaitaka Israel kuheshimu uhuru wa Lebanon na mipaka yake.
Israel na harakati ya Hizbullah walifikia makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yalianza kutekelezwa Novemba 27, 2024. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Tel Aviv ilitakiwa kuondoka kikamilifu kutoka eneo la Lebanon, lakini imebakisha wanajeshi wake katika maeneo matano, jambo ambalo ni ukiukaji wazi wa Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 1701 na masharti ya makubaliano ya Novemba yaliyopita.
Tangu kutekelezwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, Israel imekiuka makubaliano hayo mara kadhaa kwa kushambulia tena maeneo ya Lebanon.
Mamlaka za Lebanon zimesema kuwa ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano na utawala wa Israel unahatarisha uthabiti wa kitaifa.