Nakba Nyingine: UN yaonya kuhusu kuhamishwa kwa nguvu kwa Wapalestina
Kamati Maalumu ya Umoja wa Mataifa imeonya kwamba dunia inaweza kuwa inashuhudia “Nakba nyingine” huku utawala wa Israel ukiendelea na mpango wake wa kuwaondoa kwa nguvu maelfu ya Wapalestina katika ardhi yao kwenye vita vyake vya muda mrefu vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Kamati Maalumu ya Umoja wa Mataifa ya Kuchunguza Mienendo ya Israel Inayoathiri Haki za Binadamu za Watu wa Palestina na Waarabu Wengine katika Maeneo Yanayokaliwa kwa Mabavu, imesisitiza kuwa Israel inatekeleza “maangamizi ya kizazi” na kusababisha “mateso yasiyoweza kuelezeka” kwa Wapalestina.
Onyo hili limetolewa wakati ambapo utawala wa Israel umetangaza kuwa vitendo vyake vya mauaji ya kimbari huko Gaza havitaisha hadi “mamia ya maelfu” ya Wapalestina wahamishwe.
Kwa Wapalestina, kuhamishwa kwa lazima kunafufua kumbukumbu za “Nakba”, janga la mwaka 1948 ambapo mamia ya maelfu walilazimishwa kuondoka makwao kufuatia kuanzishwa kwa kile wanachokiita utawala haramu wa Israel.
Mnamo mwaka 1948, takriban Wapalestina 760,000 walifukuzwa kwa nguvu kutoka kwenye makazi yao kutokana na matukio yaliyopelekea kuvamiwa kwa Palestina na ardhi zao kukaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
“Israel inaendelea kuwasababishia watu wanaoishi chini ya uvamizi wake mateso yasiyoweza kuelezeka, huku ikizidisha unyang’anyi wa ardhi kama sehemu ya malengo yake mapana ya ukoloni,” kamati hiyo imesema katika taarifa yake.

“Tunachoshuhudia sasa kinaweza kabisa kuwa Nakba nyingine.”
Ripoti hiyo imesisitiza kuwa lengo kuu la utawala vamizi ni upanuzi wa makazi ya kikoloni, ikiongeza: “Operesheni za kiusalama zinatumika kama kisingizio cha kunyang’anya ardhi kwa kasi, kuhamisha watu kwa nguvu, kuwanyang’anya mali, kubomoa nyumba, kuwafukuza kwa nguvu, na kufanya maangamizi ya kizazi ili kubadilisha jamii za Kipalestina na kuwaweka walowezi wa Kiyahudi mahali pao.”
Vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendeshwa na Israel dhidi ya Gaza vilivyoanza Oktoba 2023 vimesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 52,787 na kujeruhi wengine 119,349. Waathiriwa wengi ni wanawake na watoto.

Mnamo Novemba 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilitoa hati za kukamatwa kwa waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na waziri wa zamani wa vita, Yoav Gallant, kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu huko Gaza.
Tel Aviv pia inakabiliwa na kesi ya mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kutokana na vita vyake dhidi ya Gaza.