Kiongozi wa kidini wa Wadruze: Hatutaki 'himaya' ya Israel
Kiongozi wa kiroho wa kabila la wachache la Druze nchini Lebanon amesema jamii hiyo inapinga ombi la utawala wa Israel la "kuwalinda" walio wachache.
Sheikh Sami Abi al-Muna ameyasema hayo katika hadhara ya maafisa wa jamii ya Druze katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut jana Ijumaa.
Alikuwa akirejelea mauaji na ukiukaji wa mara kwa mara wa ardhi ya Syria, ambao umefanywa na utawala wa Kizayuni kwa kisingizio cha "kuwalinda" Wadruze, ambao pia ni wachache nchini Syria.
Ombi la upande wa Tel Aviv "ni hatari kwa historia na utambulisho wetu," al-Muna ameongeza. Wadadisi wa mambo wanasema matamshi hayo ni onyo kwa serikali ya Tel Aviv dhidi ya kujaribu kujihusisha na jamii za walio wachache ili kuendeleza malengo yake ya kikanda ya kujitanua.
Wakati huo huo kiongozi huyo wa kiroho wa Wadruze ameashiria mapigano ya hivi majuzi kusini mwa Syria kati ya watu wa jamii ya Druze na Mabedui, ambayo hadi sasa yamepelekea watu wasiopungua mamia moja kuuawa.
Ameonya kwamba, mapigano hayo ya kimadehehebu na kikabila "yanaip Israel kisingizio cha kuingilia kati na kushadidisha hali katika eneo hilo."
Utawala huo umezidisha mashambulizi yake dhidi ya Syria tangu mwaka jana, ukidai kuwa unalenga kuzuia kuenea ghasia kutoka kwa nchi hiyo ya Kiarabu hadi katika maeneo yanayoukaliwa kwa mabavu.
Siku ya Jumatano, hujuma za Israel zilipamba moto zaidi, wakati utawala huo pandikizi ulipofanya mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo mbalimbali ya Syria, ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa Damascus.