Ishaq Dar: Pakistan hivi karibuni itakuwa mwenyeji wa Rais Pezeshkian
Ishaq Dar Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan amesema kuwa Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi karibuni atafanya ziara rasmi mjini Islamabad.
Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya al Arabiya pambizoni mwa ziara yake mjini New York, Ishaq Dar amesema kuwa Rais Pezeshkian anatazama kuitembea Pakisran na akasema anatumai kuwa ziara hiyo itafanyika mapema mwezi Agosti.
Pakistan inaunga mkono diplomasia na maamuzi ya busara katika kanda hii na wakati huo huo inakaribisha jitihada zote za kupunguza mivutano na kufanya mazungumzo na Iran.
Naibu Waziri Mkuu wa Pakistan ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje amesema amekuwa akiwasiliana kwa karibu na Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kwa sababu Pakistan ni jirani ya Iran; kwa hiyo nchi hiyo haiwezi kusalia kimya kuhusu matukio ya karibuni ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya taasisi za nyuklia za Iran.
Naibu Waziri Mkuu wa Pakistan amelaani uvamizi wa Israel dhidi ya Iran na mashambulizi ya Marekani katika vituo vya nyukia vya Iran na kusema Pakistan haiwezi kuyapuuza mashambulizi hayo hata kama yametekelezwa na nchi rafiki.
Ameongeza kuwa: Pakistan iko tayari kutekeleza juhudi za ngazi ya juu za upatanishi ili kudumisha diplomasia ya kikanda.
Esmail Baqaei Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kwa upande wake amesema kuwa Rais Pezeshkian anatazamia kufanya ziara Pakistan na kwamba ziara hiyi inadhihirisha umuhimu wa uhusiano kati ya nchi mbili.