Kwa nini Marekani inang'ang'ania Hizbullah ya Lebanon ipokonywe silaha?
Duru za habari zimetangaza kuwa Marekani imeongeza mashinikizo yake kwa Lebanon ya kuitaka ipitishe haraka iwezekanavyo kupitia baraza lake la mawaziri uamuzi rasmi unaoiwajibisha kuipokonya silaha Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa nchi hiyo ya Hizbullah.
Serikali ya Washington ilianza kuzungumzia suala la kupokonywa silaha Hizbullah tangu ulipoanza kutekelezwa usitishaji vita kati ya harakati hiyo ya Muqawama ya Lebanon na utawala wa kizayuni wa Israel. Wito huo umekuwa ukifuatiliwa kwa uzito zaidi tokea Donald Trump aingie madarakani nchini Marekani, na mashinikizo ya Washington dhidi ya serikali ya Beirut juu ya suala hilo yameongezeka pia. Hatua hiyo imegeuzwa hata kuwa sharti la kuanza tena mazungumzo ya kusitisha operesheni za kijeshi za utawala wa kizayuni ndani ya ardhi ya Lebanon.
Suali muhimu la kujiuliza hapa ni, kwa nini Marekani inang'ang'ania Hizbullah ipokonywe silaha; na kuna malengo gani ambayo serikali ya Washington inayafuatilia katika kadhia hiyo?
Sababu na lengo muhimu zaidi la Marekani la kung'ang'ania Hizbullah ipokonywe silaha ni kufuatilia na kufanikisha maslahi ya utawala wa Kizayuni. Utawala wa Kizayuni wa Israel unadai kuwa unaanzisha nidhamu mpya ya kikanda katika eneo la Asia, nidhamu na utaratibu ambao utaambatana na utawala huo ghasibu kulihodhi na kulidhibiti eneo hili. Kwa ajili ya kufanikisha mpango huo, Israel inataka kuhakikisha unaudhoofisha Mhimili wa Muqawama; na Marekani kwa upande wake inafanya juu chini ili kufanikisha ajenda hiyo ya Wazayuni.
Hata kama katika mazungumzo na viongozi wa serikali ya Lebanon Marekani imedai kwamba kuipokonya silaha Hizbullah na kuhakikisha silaha zote zinakuwa mikononi mwa jeshi kunadhamini maslahi ya Beirut, lakini ukweli ni kwamba Washington haifikirii kitu kingine chochote isipokuwa maslahi ya Tel Aviv. Kuhusiana na hilo, afisa mmoja wa Hizbullah anayehusika na masuala ya Bunge amesema: "Wamarekani hawafanyi chochote kwa maslahi ya Lebanon, bali wanahudumia maslahi ya Israel. Wanataka kulazimisha mambo kwa amri na mabavu. Wanaitaka Lebanon itekeleze majukumu yake yote, lakini mkabala wake hawaitaki Israel ifanye chochote".

Sababu nyingine muhimu ya ung'ang'anizi wa Marekani wa kupokonywa silaha Hizbullah ni kuiingiza Lebanon kwenye mkondo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni. Kwa hakika, kuipokonya silaha Hizbullah ni sawa na kuuondolea kitisho utawala wa Kizayuni na kurahisisha suala la Lebanon kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo haramu.
Kuanzisha Lebanon uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni kuna umuhimu mkubwa kwa utawala huo kwa sababu Hizbullah, ambayo hivi sasa ina nafasi kubwa katika muundo wa madaraka wa Lebanon, inahesabiwa kuwa ni miongoni mwa wanachama muhimu zaidi wa Mhimili wa Muqawama.
Lengo jengine muhimu inalofuatilia Marekani ni kuathiri hali ya kisiasa na kiusalama ya ndani ya Lebanon. Kwa upande mmoja, Washington inajaribu kuzusha mpasuko kati ya Hizbullah na vyama na mirengo mingine ya kisiasa ya Lebanon, na kwa upande mwingine, inafanya kila njia ili kupunguza uzito wa nafasi ya kisiasa ya Muqawama wa Lebanon kwa kudai Hizbullah ipokonywe silaha hata kama pendekezo hilo halitatekelezwa; na kwa kufanya hivyo kuleta mabadiliko makubwa katika uga wa siasa za nchi hiyo. Kuhusiana na suala hilo, afisa wa Hizbullah wa masuala ya Bunge amesema, malengo ya Washington na Israel iliyo nyuma yake yako wazi kabisa. Wanataka kuiangamiza Hizbullah na kuwaweka Walebanon kwenye makabiliano na harakati hiyo kwa kuitishia Lebanon kwamba itapoteza fursa na itakabiliwa na matokeo mabaya endapo Hizbullah haitakabidhi silaha zake.
Hizbullah kwa upande wake imetoa mjibizo kwa dai hilo la Marekani. Katika salamu na ujumbe mpya iliomfikishia Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berri, harakati hiyo ya Muqawama imetangaza na kusisitiza kwamba, hata kama Israel itaondoka kusini mwa Lebanon, haitakuwa tayari kwa namna yoyote ile kukabidhi silaha zake.../