Pep Guardiola: Ubinadamu umetoweka mbele ya maafa ya Gaza
Kocha wa timu ya soka ya Manchester City Pep Guardiola kwa mara nyingine tena amekosoa vikali ukimya wa walimwengu kuhusiana na jinai za utawala wa kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kusema: "Ubinadamu umetoweka."
"Sote tunatazama maafa haya mubashara, lakini hatuonyeshi mwitikio wowote wa kweli. Hii ni ishara ya kutoweka kwa ubinadamu wetu kwa pamoja," alisema koccha huyu mashuhuri wa soka katika mahojiano na jarida la Uhispania la GQ.
Guardiola aliongeza: "Inaonekana kwamba watu hawana ubinadamu tena uliobaki, iwe Ukraine au Palestina. Hatufanyi lolote kuhusu mkasa huu na tunaendelea kucheza kana kwamba hakuna kilichotokea."
Akiashiria Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia, Pep Guardiola alisema, "Hapo zamani, majanga yaliendelea kufichwa, lakini leo tunaona kila kitu mubashara kwenye televisheni, lakini hatuna majibu hata kidogo."
Hii si mara ya kwanza kwa kocha huyo wa timu ya soka ya Manchester City kuwaunga mkono watu wa Palestina; hapo awali alizungumza kuhusu haja ya kutetea haki na haki za binadamu duniani kote katika sherehe ya digrii ya heshima kutoka Chuo Kikuu cha Manchester mwezi Juni.
Katika hotuba yake ya kupokea heshima hiyo, Guardiola alisimama kidete kwa ajili ya watu wa Gaza. Alilaani kile alichokiita mateso ya wazi yanayoendelea kufanywa na Israel katika vita vinavyoendelea huko Gaza.
Akizungumzia watoto wake watatu – Maria, Marius na Valentina – Guardiola alisema kwamba kila asubuhi “tangu jinamizi lilipoanza” Gaza, kila anapowaona mabinti zake wawili na mwanawe wa kiume, anakumbuka watoto wa Gaza, jambo ambalo humfanya “kuhisi hofu kubwa sana.”