Hamas yapongeza 'ujasiri' wa mawaziri wa Uholanzi kujiuzulu juu ya Gaza
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imepongeza hatua ya kujiuzulu mawaziri kadhaa wa Uholanzi, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Caspar Veldkamp, kujibu hatua ya kukataa kwa serikali yao kuiwekea vikwazo Israel. Hamas imetaja kujiuzulu huko kama uamuzi wa kijasiri na wa kimaadili.
Katika taarifa yake, Hamas imesisitiza kwamba msimamo wa kupigiwa mfano uliochukuliwa na mawaziri waliojiuzulu wa Uholanzi unaakisi maadili ya kibinadamu na unathibitisha tena namna wanavyotii sheria za kimataifa, hasa kwa kuzingatia janga la kibinadamu linaloendelea kuwakabili watu wa Gaza.
Harakati hiyo ya kupigania ukombozi wa Palestina imetaja kujiuzulu kwao kuwa ni msimamo wa kimaadili unaofanyika wakati Umoja wa Mataifa umetangaza baa la njaa katika Ukanda wa Gaza.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi alijiuzulu siku ya Ijumaa baada ya kushindwa kupata uungwaji mkono wa baraza la mawaziri kwa vikwazo zaidi dhidi ya Israel, kutokana na mashambulizi ya kijeshi ya utawala huo wa Kizayuni huko Gaza.
Alisema amejiuzulu kwa kuwa hajaweza kufikia makubaliano juu ya "hatua za maana" juu ya vikwazo vipya, na mara kadhaa amekabiliana na upinzani kutoka kwa wenzake juu ya vikwazo vilivyowekwa tayari. Juhudi zake ni pamoja na kuwapiga marufuku mawaziri wa mrengo wa kulia wa Israel, Bezalel Smotrich na Itamar Ben-Gvir kuingia nchini humo, akiashiria nafasi zao katika kuchochea ghasia za walowezi wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.
Veldkamp pia ilibatilisha vibali vitatu vya usafirishaji wa vifaa na vipuri vya meli za jeshi la wanamaji, akionya kuhusu "hali mbaya" huko Gaza, na "hatari ya matumizi yake yasiyofaa".
Kufuatia kujiuzulu kwake, mawaziri wote wa chama chake cha kisiasa cha New Social Contract na makatibu wa serikali wametangaza uungaji mkono wao kwa Veldkamp na kujiuzulu kutoka kwa serikali ya muda, kuonyesha mshikamano na mwenzao.