Mawaziri wa kizayuni watoa msimamo kuhusu Ghaza: "Wazingireni, waacheni wafe kwa njaa"
Mawaziri wa utawala wa kizayuni wa Israel wenye misimamo mikali ya chuki wametetea waziwazi hatua ya kuwatesa kwa njaa Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza.
Bezalel Smotrich na Itamar Ben Gvir wametoa msimamo huo wakati walipokuwa wakizungumza katika kikao cha baraza la mawaziri la Israel, na kuzua majibizano makali baina yao na mkuu wa majeshi Eyal Zamir juu ya mkakati wa vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na utawala wa kizayuni dhidi ya eneo hilo la Palestina lililowekewa mzingiro.
Kwa mujibu wa chaneli ya 12 ya Israel, katika kikao hicho waziri wa fedha Bezalel Smotrich alilitaka jeshi lichukue hatua kali dhidi ya Wapalestina waliosalia katika maeneo yao na kukataa kuhama.
"Tulikuamuru (kufanya) operesheni ya haraka. Kwa maoni yangu, unaweza kuwawekea mzingiro. Yeyote asiyehama msimwache hivi hivi. Msiwape maji wale umeme - wafe kwa njaa au wasalimu amri. Hiki ndicho tunachotaka, na wewe unao uwezo (kufanya)", amenukuliwa akisema waziri huyo mzayuni wa mrengo wa kulia mwenye misimamo mikali ya chuki dhidi ya Wapalestina.
Kwa mujibu wa chaneli ya 12 ya Israel majibizano hayo yalipamba moto wakati waziri wa usalama Itamar Ben Gvir alipoingilia kati, akimtuhumu mkuu wa majeshi kuwa anasitasita kutekeleza operesheni ya kuikalia Ghaza kikamilifu na kumuuliza kama ni kwa sababu ya "kumuogopa wakili mkuu wa jeshi."
Naye Smotrich akafuatia na kumtuhumu Zamir kuwa anakaidi amri za kisiasa na kuzuia kuchukuliwa hatua madhubuti, akisema: "hivi sivyo uongozi wa kisiasa ulivyoamuru. Hutaki kuwashinda [Hamas]."
Kwa mujibu wa duru za kizayuni, Zamir alijibu kwa kusema: "nyinyi hamuelewi chochote. Hamujui brigedi na batalioni ni kitu gani. Hili linachukua muda."
Wakati huohuo mkuu wa majeshi ya utawala wa kizayuni wa Israeli Eyal Zamir ametoa wito kwa waziri mkuu Benjamin Netanyahu akubali pendekezo la sasa la kusimamisha vita na kubadilishana wafungwa, akionya kwamba kuukalia kikamilifu Mji wa Ghaza kunasababisha "hatari kubwa" kwa maisha ya mateka.
Chaneli ya 13 ya Israel imemnukuu Zamir akisema: "kuna mpango uko mezani, na inapasa ufanyiwe kazi hivi sasa hivi".
Kupitia taarifa yake, mkuu wa majeshi ya utawala wa kizayuni amesema, msimamo wake unaakisi matakwa ya Waisrael waliowengi ambayo ni kufikiwa makubaliano kamili yatakayowezesha kurejeshwa mateka 50 na kuhitimishwa vita.../