Hamas yakadhibisha madai ya kuuawa kigaidi Khalil al-Hayya
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130056-hamas_yakadhibisha_madai_ya_kuuawa_kigaidi_khalil_al_hayya
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imepinga madai ya utawala haramu wa Israel kwamba umemuua kigaidi Khalil al-Hayya, mmoja wa viongozi waandamizi wa kundi hilo la Muqawama.
(last modified 2025-08-27T10:22:42+00:00 )
Aug 27, 2025 10:22 UTC
  • Hamas yakadhibisha madai ya kuuawa kigaidi Khalil al-Hayya

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imepinga madai ya utawala haramu wa Israel kwamba umemuua kigaidi Khalil al-Hayya, mmoja wa viongozi waandamizi wa kundi hilo la Muqawama.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Hamas amekanusha vikali ripoti hizo zinazodai kuuawa shahidi Khalil al-Hayya, Mkuu wa Ofisi ya harakati hiyo huko Gaza, ambaye pia ni mpatanishi mkuu wa mazungumzo ya usitishaji vita.

Shirika la habari la Mehr limemnukuu afisa huyo wa Hamas akipuuzilia mbali madai hayo, aliyoyataja kuwa propaganda za maadui, akisisitiza kwamba Khalil al-Hayya bado yuko hai na anaendelea na majukumu yake.

Afisa huyo wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amezitaja tetesi hizo kuwa ni sehemu ya vita vya kisaikolojia na vyombo vya habari vya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina na viongozi wa Muqawama.

Haya yanajiri huku utawala huo pandikizi ukishadidisha mashambulizi yake ya kinyama katika vita vyake vya mauaji ya halaiki vilivyoanza Oktoba 2023 katika Ukanda wa Gaza.

Huku hayo yakiarifiwa, Ofisi ya Kisiasa ya Hamas imetangaza kuwa, harakati hiyo itakabiliana vikali na senario  zozote tarajiwa za adui, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mpango wa utawala haramu wa Israel wa kuukalia kwa mabavu Ukanda wa Gaza.

Hamas imesisitiza kuwa, "Chaguo la Muqawama linabakia pale pale maadamu uvamizi huo utaendelea, na ingawa takwa letu kuu ni kusimamishwa vita na kumalizika uchokozi, lakini ikiwa vita vitalazimishwa juu yetu, hatutakuwa na budi ila kutetea watu na ardhi yetu."